STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21 Novemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wazazi wametakiwa kubadilika na kuwapokea tena katika jamii vijana walifanikiwa kuacha matumizi ya madawa ya kulevya.
Wito
huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na vijana walioko
katika makazi ya vijana walioamua kuacha madawa ya kulevya huko Limbani,
Wilaya ya Wete Mkoa wa Kuskazini Pemba.
Katika
risala yao kwa Rais vijana hao walieleza kuwa moja ya matatizo
wanayowakabili baada ya kufanikiwa kuacha madawa hayo ni kukataliwa na
wazazi na kutotazwa vyema na jamii.
“wazazi
hawana budi kukumbuka kuwa vijana hao ni watoto wao waliowazaa, kuwalea
na kwamba pale mtoto anapopotoka na baadae kujirudi ni wajibu wao
kuwapokea tena na kuwapa upendo kama zamani” alisema Dk. Shein.
Rais
alieleza kuwa ametiwa moyo na mipango mizuri ya vijana hao kuwa
Serikali ina kila sababu ya kuwaunga mkono na ni wajibu wake kama mlezi
wa raia wote.
“Serikali
ina kila sababu za kuwasaidia katika maisha yenu.Tunahitaji kuwaleta,
kuwaenzi na kuwapa huduma kama walivyo wananchi wengine”alibainisha Dk.
Shein.
Alimpongeza
mwanzilishi wa nyumba hiyo ambazo hadi sasa zimefikia saba kisiwani
Pemba bwana Abdulwahid Salim kwa uamuzi wake wa busara baada ya kufaulu
kujitoa katika matumizi ya madawa ya kulevya kurejea nyumbani kutoka
nchini Kenya ili kusaidia ndugu zake walioathirika.
“Tunampongeza na kumshukuru ndugu yetu Abdulwahid
ambaye mara baada ya kuyashinda madawa ya kulevya huko nchini Kenya
alikokuwa akiishi aliamua kurejea nyumbani kusaidia ndugu zake
walioathirika na madawa hayo”Dk. Shein alisema.
Alisisitiza
kuwa si jambo la busara hata kidogo kuwalaumu vijana hao kwa
yaliyowakuta badala yake jamii iwaunge mkono katika harakati zao za
kurejea katika maisha yaoe ya kawaida.
Akijibu
maombi ya vijana hao Rais aliahidi kuwapatia kompyuta mbili ndogo
(laptop) na magodoro 30 pamoja kuielekeza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais kuangalia namna ya kuongeza bajeti ya huduma za nyumba hizo.
Halikadhalika
Dk. Shein aliwaahidi kuwasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
kuangalia namna ya kutekeleza ombi lao la kupewa fursa za kutoa elimu
dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya maskulini.
Kuhusu
suala la kuwezeshwa aliwataka vijana hao kutumia fursa zinazotolewa na
Serikali za uwezeshaji kwa njia ya mikopo ili nao waweze kufaidkka na
huduma hizo kama wananchi wengine.
Akizungumza
kabla Kiongozi wa Nyumba hiyo Bwana Abdulwahidi Salim alieleza kuwa
kazi wanayoifanya katika nyumba hizo ya kiroho ya kuwarejesha vijana
maisha yao ya kawaida na kuacha tabia ambazo zinaikera jamii ambazo
ndizo zinazoifanya jamii kuwachukia na hata kukata kuwapokea tena katka
jamii.
“Tumekuwa
tukifanya kazi ya kuwafanya vijana hawa sio tu kuacha madawa lakini pia
kuacha tabia chafu inazoichukiza jamii kama wizi, mauaji, ugomvi na
uzinzi ambao unasababisha kusambaza virusi vya ukimwi” Alieleza
Abdulwahid na kuvuta hisia za wananchi na viongozi waliokuwepo.
Awali
akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Uratibu na
Udhibiti wa Madawa ya Kulevya Bi Kheriyangu Mgeni Khamis alieleza kuwa
Ofisi yake kwa kushirikiana na uongozi wa nyumba hizo wanaandaa muongozo
wa namna ya kuendesha nyumba hizo ili kuweka taratibu na mwenendo
unaofanana.
Alieleza
kuwa katika kukabiliana na tatizo la jamii kuwakataa vijana hao
wameanzisha mpango wa kutoa ushauri nasaha kwa jamii kwa kuwatumia
vijana hao ili kuivuta jamii kuona kuwa vijana hao bado ni sehemu ya
jamii na wana mchango kusadia jamii yao.
0 comments:
Post a Comment