Home » » Maalim Seif: Harakati za kudai Z`bar huru zilianza wakati wa Mzee Karume

Maalim Seif: Harakati za kudai Z`bar huru zilianza wakati wa Mzee Karume

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi(CUF),Maalim Seif Sharif Hamad
 
Katibu  Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, amesema harakati za kudai mamlaka kamili kwa Zanzibar hazikuanza sasa, bali zimekuwapo tangu awamu ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika  Donge Muwanda Wilaya ya Kaskazini B, visiwani hapa, Maalim Seif  alisema kwa miaka mingi, Wazanzibari wamekuwa wakilalamikia kubanwa katika mambo mbalimbali muhimu kwa ustawi wao.

Aliitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuweka mipaka ya Zanzibar na Tanzania Bara ili kupata katiba yenye maslahi kwa pande zote na kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Aidha, alishauri kuwa katiba hiyo lazima ieleze uraia ambao ndiyo kielelezo cha uzalendo na kudhibiti uhamiaji haramu katika visiwa vya Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alieleza kuridhishwa na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kufanya marekebisho katika Muswaada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na Wazanzibari kutoshirikishwa katika hatua za awali kabla ya kupelekwa Bungeni.

Katika mkutano huo, CUF ilipokewa wanachama wapya 240 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwamo mjumbe wa Mkutano mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B”, Salim Khamis Amour, ambaye alitoa siri za chama chake wakati akihutubia mkutano huo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa