Home » » Zanzibar yashauriwa kuondoa urasimu wa kibiashara

Zanzibar yashauriwa kuondoa urasimu wa kibiashara

Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar, imeshauriwa kuondoa urasimu katika kusajili biashara na kuimarisha miundombinu inayohusisha wafanyabiashara wadogo na wa kati, ambao ndiyo tegemeo kubwa la wananchi. 

Ushauri huo umekuja baada ya utafiti wa kutambua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara Zanzibar akielezea muhtasari huo kwa waandishi, Makamo wa Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Viwanda na Wakulima, Ali Aboud Mzee.

Alisema serikali lazima iwekeze zaidi kwa wafanyabiashara na kuangalia uwezekano wa kupunguza utitiri wa kodi na badala yake kutanua wigo wa nafasi za kukopa bila ubaguzi, na kutoa elimu bora kwa wafanyabiashara nchini. Alisema licha ya kuwapo na mabadiliko ya sera ya biashara ndogondogo na za kati, bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wafanyabiashara visiwani hapa.

Alisema wafanyabiashara, wamekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa miundombinu, urasimu wa kusajili biashara na ugumu wa kupata mikopo.
“Hali iliyopo sasa ya utitiri wa kodi inasababisha biashara nyingi kufa na kuwabakisha wananchi katika umasikini," alisema Aboud.

Hata hivyo, alisema jitihada zilizochukuliwa na serikali kutunga sera ya kuendeleza biashara ndogondogo ni nzuri, lakini utekelezaji wake hauridhishi.  Aliitaka serikali kuzipatia ufumbuzi changamoto za sekta hiyo ambayo inaendesha asilimia 88 ya biashara zote zilizopo Unguja na Pemba, na kuajiri wananchi 117,020.

Mkurugenzi wa jumuiya hiyo, Munira Humud, alisema wafanyabiashara wa sekta hiyo wana nafasi kubwa ya kuinua uchumi wa nchi iwapo watawekewa mazingira mazuri.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa