Taasisi inayosimima uhifadhi
na matengenezo ya nyumba za Serikali imeshauriwa kuifanyia marekebisho
yaliyosalia Ikulu ndogo ya Kibweni ili itumike vyema katika maadhimisho ya
Sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Ushauri huo umetolewa na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara
fupi ya kuikagua nyumba hiyo iliyopo pembezoni mwa Makao Makuu ya Kikosi
cha kuzuia Magendo Zanzibar { KMKM } Kibweni Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Balozi Seif ambaye
ameridhika kiasi na hali halisi ya mazingira ya Ikulu hiyo alisema ni
vyema nyumba hiyo ya Serikali ikapangiwa taratibu za kutumika
badala ya kuachwa ikikaa bure .
Amesema Serikali katika
kipindi kirefu imekuwa ikipokea wageni wa Kitaifa na Kimataifa wenye hadhi ya
kuishi kwenye nyumba hiyo lakini wengi kati yao wanaishia kuwekwa katika
Hoteli za Kitalii jambo ambalo linaweza kuepukwa.
Amewataka wahusika wa
matengenezo ya nyumba za Serikali kuhakikisha kwamba nyumba hiyo {
Ikulu } inakamilishwa hitilafu ndogo ndogo zilizobakia ili iweze
kuhudumia wageni watakaoalikwa kuhudhuria maadhimisho ya sherehe za
Mapinduzi kutimia Nusu Karne.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliwapongeza wasimamizi wa Ikulu hiyo ya Kibweni kwa
hatua wanazozichukuwa katika kuihudumia nyumba hiyo kongwe.
Alisema mazingira
bora yaliyopo hivi sasa kwenye nyumba hiyo yanaruhusu kwa baadhi ya
Mikutano na Kazi za Viongozi Wakuu wa Serikali kuzifanyiwa katika
eneo hilo.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya
Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Nd. Salum Maulid alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba tatizo liliopo hivi sasa katika nyumba hiyo ni
marekebisho ya jiko la kupikia pamoja na huduma ya maji ambayo haipatikani
kikawaida.
Nd. Salum alisema
huduma hiyo ya maji safi hupatikana kwa nadra katika kipindi kirefu
tatizo ambalo linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina na kulitafutia ufumbuzi wa
kudumu.
0 comments:
Post a Comment