Home » » 'Wazanzibari tumieni vema fursa za Muungano'

'Wazanzibari tumieni vema fursa za Muungano'

WAZANZIBARI wametakiwa kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kutumia vizuri fursa za kiuchumi ambazo ni kubwa, zitakazowakomboa vijana kuachana na ajira za serikali. Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud wakati akifungua Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Zanzibar kuhusu faida za Muungano na hasara zake kama ukivunjika.
Alisema Wazanzibari wanayo kila aina ya fursa katika Muungano uliopo sasa kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi, kama wanavyotumia baadhi ya wananchi wa Zanzibar waliopo Tanzania Bara, ambao wamewekeza katika miradi mbalimbali, ikiwemo biashara.
“Faida za Muungano uliopo sasa ni kubwa sana kuliko hasara za kuvunjika kwa Muungano huo....Wazanzibari wanatakiwa kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo sasa kwa ajili ya kujiendeleza,” alisema.
Akifafanua, Aboud alisema Muungano uliopo sasa, una changamoto nyingi ikiwemo kero, ambazo zimekuwa zikiyumbisha Muungano huo, lakini hata hivyo alisema faida za Muungano ni kubwa.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Ali Salim alikiri kuwepo kwa fursa nyingi za Muungano ambapo Zanzibar inaweza kufaidika nazo, lakini akasema Serikali zote mbili zinatakiwa kuziainisha kwa wananchi.
Kwa mfano, alisema Wazanzibari wanao uwezo mkubwa wa kuwekeza sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano pamoja na kufanya biashara bila ya vikwazo kama ilivyo sasa.
“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar faida zake ni kubwa zaidi kwa Zanzibar yenye idadi ndogo ya watu wa wastani milioni moja na laki tatu kulitumia soko kubwa la Tanzania Bara lenye zaidi ya watu milioni 43,” alisema.
Fatma Mohamed mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Tunguu, anayesomea Sheria, alisema ukosefu wa elimu kuhusu faida za Muungano zinazopatikana kwa pande mbili, zimewafanya baadhi ya watu kuona Muungano huo hauna faida.
Kwa mfano, alisema Wazanzibari wanafaidika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali mbili, ambapo mwanafunzi kutoka Zanzibar anaweza kuomba mkopo wa elimu ya juu katika Bodi ya Mikopo ya Muungano.
“Hizi fursa zilizopo kama Wazanzibari watazichangamkia vizuri, basi wanayo nafasi kubwa ya kupiga hatua ya kiuchumi na maendeleo ikiwemo Sekta ya Uwekezaji,” alisema.
Kongamano hilo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ni sehemu ya makongamano mbalimbali yatakayoendeshwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ambayo lengo lake ni kutoa elimu zaidi kuhusu faida za Muungano. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utafikisha miaka 50 mwakani. Uliasisiwa Aprili 26, mwaka 1964.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa