“Lengo ni kuunda katiba yenye masilahi ya nchi na si watu au kikundi cha
wachache, jukumu lililobaki ni la wananchi wenyewe kupitia kwa
wawakilishi wao kabla ya kupigwa kura ya maoni,”
Kikwete
Zanzibar. Rais Jakaya Kikwete, amesema Bunge la
Katiba ndilo litakalotoa uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba Mpya kabla ya
kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo jana katika viunga vya Maisara Suleiman.
Msimamo huo umekuja huku vyama vikuu vya siasa visiwani Zanzibar vikitofautiana kuhusu yaliyoko katika Rasimu ya Katiba Mpya.
Kwa upande wake, CCM inapinga mfumo wa Serikali tatu wakati CUF inaunga mkono mapendekezo hayo.
Rais Kikwete alisema Tume ya Jaji Warioba imemalizika kazi zake na kwamba kazi ya msingi sasa imeanza.
Alisema wananchi bado wana nafasi ya kutoa maoni
yao kupitia kwa wabunge na wawakilishi wao na kwamba uamuzi wa mwisho ni
wao kwa kupiga kura ya maoni.
“Kazi ndiyo kwanza imeanza, mkoko ndiyo unaalika
maua, wananchi wenyewe wataamua kwa hiari yao lipi litafaa na lipi
halihitajiki kuwekwa kwenye kwenye Katiba Mpya, hebu kaeni na wabunge
wenu mjitosheleze, semeni bila ya kificho, mnataka lipi na lipi
hamkubaliani nalo,” alisema Rais Kikwete.
Aidha, alisema kuna baadhi ya watu bila aibu
wanapita mitaani wakipotosha kwamba Katiba Mpya imekamilika jambo ambalo
si la kweli.
Alisema baada ya kuwasilishwa kwa rasimu ya pili,
hatua inayofuata ni rasimu hiyo kutajadiliwa na Bunge la Katiba na
kufuatiwa na kura ya maoni.
Rais Kikwete alisema wananchi wana nafasi ya
kuendelea kutoa maoni yao ili kupata katiba safi na kwamba si lengo la
taifa kuunda Katiba itokanayo na kundi fulani.
“Lengo ni kuunda katiba yenye masilahi ya nchi na
si watu au kikundi cha wachache, jukumu lililobaki ni la wananchi
wenyewe kupitia kwa wawakilishi wao kabla ya kupigwa kura ya maoni,”
alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,
Rais Kikwete aliwahimiza vijana kuyathamini na kuyaenzi kwa kuzingatia
kuwa yameondosha dhuluma na ukandamizaji uliofanywa na utawala wa
kisultan.
“Mapinduzi ya Zanzibar ndiyo ukombozi na uhuru kamili, hata
waliokuwa wakikandamiza wenzao nao walikombolewa na kujitambua. ASP
ilijenga nchi isiyokuwa na uonevu wala ukandamizaji, kikaleta usawa na
uhuru kamili,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Khamis
Juma alimkumbusha Rais Kikwete kuwa nia njema ya CCM ya kukubali
maridhiano ya kisiasa haijaheshimiwa na wapinzani wao Zanzibar.
Alisema hali hiyo inadhihirishwa na kejeli dhidi ya mapinduzi na watu kutaka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Sadifa alisema UVCCM haitakubali kusimama na
kiongozi yeyote wa kisiasa au kiserikali mwenye nia ya kuvunja Muungano
au kuyasaliti Mapinduzi ya Zanzibar.
Akisoma taarifa fupi, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM
Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka alisema maoni ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ya Jaji Warioba hayakubaliki na yamekosa mashiko, uzalendo na
nguvu ya kudumisha umoja wa Kitaifa.
chanzo;Mwananchi
chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment