WATU
sita wamefariki dunia na wengine watatu kuokolewa katika boti ya abiria
ya MV Kilimanjaro iliyokumbwa na dhoruba ya mawimbi makali kutokana na
kuchafuka kwa hali ya hewa baharini.
Ajali hiyo ilitokea jana katika eneo la mkondo wa Nungwi wakati boti hiyo ikitoka Pemba kurudi Unguja.
Naibu
Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo ambapo watoto watatu wamefariki dunia pamoja na
wanawake watatu wenye umri kati ya miaka 36-50.
Kamishna
wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alithibitisha ajali
hiyo na kusema uchunguzi zaidi unafanywa. Inadaiwa baada ya kuchafuka
kwa bahari, wimbi moja lilipiga sehemu ya mbele ya boti na abiria
waliokaa mbele walirushwa na kudondoka baharini.
Awali
Ussi aliwataka wamiliki wa vyombo vya baharini vya aina mbali mbali
kuchukua kila aina ya tahadhari zaidi katika kipindi hiki ambapo hali ya
bahari imechafuka na kuibuka kwa mawimbi makubwa.
Familia
mia mbili Wakati huo huo, zaidi ya familia mia mbili hazina makazi ya
kuishi baada ya nyumba 24 kuteketea kwa moto huko Shumba mjini katika
Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkuu wa Mkoa huo, Dadi
Faki Dadi alithibitisha kutokea kwa moto huo ambao chanzo chake
kinasadikiwa kuwa, watoto walikuwa wakipika chakula.
Dadi
alisema nyumba 14 zimeteketea moja kwa moja na moto huo, huku nyingine
10 zikiezuliwa mapaa yake na wananchi kwa ajili ya kuchukua tahadhari
ili moto usisababishe madhara zaidi.
Makamo
wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alifika kuwapa pole wananchi wa
kijiji hicho ambao wamepata mkasa wa nyumba zao kuteketea kwa moto.
Alisema
kazi inayofanywa kwa sasa na Idara ya Maafa ni kufanya tathmini ya
nyumba zote na hasara hiyo kwa ajili ya kutoa fidia ili wananchi warudi
katika makazi mapya.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment