Zanzibar. Wabunge na Wawakilishi wa CCM
Zanzibar tayari wamekutana na kupanga mkakati wa pamoja kwa nia ya
kupinga Mfumo wa Muungano wa Serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
imefahamika juzi visiwani Zanzibar.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa kikao hicho
kilifanyika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwanduwi kuanzia saa 9.00 Alasiri hadi
saa 1:00 ya usiku chini ya Uenyekiti wa Makamo wa Pili wa Rais, Balozi
Seif Ali Iddi na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali
Vua.
Vyanzo mbalimbali vya habari kutoka ndani ya kikao
hicho vinaeleza kwamba, wabunge hao wa Bunge la Katiba walipokea
msimamo wa chama chao na kutakiwa kuutetea kwa umoja wao watakapojadili
rasimu hiyo.
Baada ya kuwasilishwa ajenda hiyo kikaoni, wajumbe
mmoja baada ya mwingine walitoa maoni yatakayofanikisha kufuzu kwa
mkakati huo huku wengine wakishauri wajumbe wapewe nafasi ya kuijadili
rasimu kupitia semina ili kujua ni maeneo gani yana manufaa na hasara.
Imeelezwa Mwakilishi Hamza alisema kutokana na
umuhimu wa rasimu hiyo,waandaliwe semina maalumu ili kukijadili kwa kina
kifungu baada ya kifungu kabla ya kufikia uamuzi wa kupitisha na
kutopitisha mambo yasiyokuwa na manufaa kwa Zanzibar na Usalama wa
Muungano wenyewe.
Alisema suala la Katiba halipaswi kujadiliwa
haraka,linahitajika umakini kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake na
kukiomba chama hicho kitayarishe semina hiyo ya uchambuzi, kujenga uwezo
na ufahamu kabla ya Bunge la Katiba halijakutana na kujadili rasimu
hiyo.
Hata hivyo kwa upande wake, Asha Bakari aliweka
wasiwasi wake kwa wajumbe kuhusu kukosa msimamo wa pamoja na kutaka kila
mjumbe aulizwe kama anataka Serikali tatu au mbili badala ya kuja
kupanga na baadaye kusalitiana mbele ya safari na kuhatarisha misingi ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo, mfanyabiashara maarufu na Mbunge wa
Mpendae ,Salum Turkey alisema kutokana na uzito wa suala la mfumo wa
Muungano ni vizuri kukafanyika kisomo maalumu (halbadiri) na mjumbe
yoyote atakayekwenda kinyume na msimamo wa chama apate laana duniani na
akhera.
Wazo hilo licha ya kuwashtuwa baadhi ya wajumbe,
wengi walionekana kukubaliana naye ili mkakati wa chama hicho uweze
kufikiwa huku Waziri wa zamani,Hamza Hassan akisisitiza rasimu yote ya
katiba ichambuliwe yanayokubalika na yasiyokubalika kabla ya Bunge la
Katiba kukutana mwaka huu.
Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai hakuweza kupatikana kuelezea kikao hicho na maazimio
yaliyofikiwa baada ya kuulizwa kwa njia ya simu na kueleza yupo katika
kikao na atafutwe muda mwengine mara baada ya kikao hicho.
Vuia aliwahi kutoa msimamo wake wakati akifungua mkutano wiki mbili zilizopita akisema atakuwa wa mwisho kuafiki.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment