Zanzibar. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema
mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar umedumaza dhana ya
demokrasia ya vyama vingi na kuficha misingi ya utawala bora kutokana na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria
viongozi waliohusika na ufisadi visiwani hapa.
Tamko hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf wakati akimnadi mgombea wa chama
hicho Jimbo la Kiembesamaki, Hasimu Juma Issa katika mkutano wa hadhara
wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Kiembesamami kisiwani Unguja.
Hamad alisema, kuundwa kwa Serikali hiyo mwaka
2010 taswira ya upinzani wa kweli imepotea na kutoweka na sasa viongozi
waliounda umoja huo wakionekana kutetea masilahi binafsi na kuwasahau
wananchi wanaoishi kwa dhiki, shida na njaa.
Alisema hata Kamati za Baraza la Wawakilishi
zinapofanya uchunguzi na kugundua vitendo vya ufisadi uliofanywa na
baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali, hakuna hatua za kisheria
zinazochukuliwa.
“Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeshindwa
kufuata nyayo za Bunge la Muungano ili kuchunguza mambo yanayolirudisha
nyuma Taifa na kuyasimamia. Ni Baraza la Washirika wa vyama vya CCM na
CUF, kuna ufisadi unaofumbiwa macho na vigogo hawajali maisha ya
wanyonge,” alisema Hamad.
Miongoni mwa ripoti za ubadhirifu wa fedha za umma
alizozitaja ni pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Baraza la
Manispaa ya Mji wa Zanzibar (ZMC) mbali na ripoti za uchunguzi wa uuzaji
wa majengo ya Serikali yaliouzwa kwa bei ya kutupwa kinyume na sheria.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema Zanzibar
alisema, vyama vya CCM na Cuf vimepoteza mwelekeo na wakati mwafaka
umefika kwa wananchi wa Zanzibar kuamua kupatikana chama mbadala
kitakachopigania masilahi ya wananchi na kuibana Serikali ndani ya nje
ya vikao vya baraza.
Kwa upande wa mgombea uwakilishi, Hasim Juma Issa
alisema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi atajenga
hospitali itakayotoa huduma zote ikiwamo uzazi na upasuaji na kuwataka
wananchi kumuunga mkono ili kuyafikia malengo yake.
Alisema hataogopa kuibana SMZ na kuongeza kasi ya
uwekezaji katika sekta ya viwanda vidogovidogo na kuishangaa Serikali ya
Mapinduzi ikikosa viwanda na kuongeza kasi ya uvuvi huku ikizungukwa na
rasilimali ya bahari.
Zanzibar,hapa upinzania umekufa,wakubwa
wanaitafuna nchi na umaskini unazidi kukithiri,vikataeni vyama vya CCM
na Cuf,vimepoteza imani yake kwa jamii,”alisema Hasim.
Alisema pamoja na wawakilishi wa Cuf na CCM
kuendelea kupokea ruzuku toka SMZ wameshindwa hata kujenga ofisi za
majimbo pia fedha wanazopewa na Serikali wameshindwa kuzifanyia
marejesho ya matumizi yake na kuahidi akishinda ataanzisha ofisi
itakayofanya kazi hadi siku za mapumziko.
Pia alisema wananchi wengi wa Kiembesamaki hutumia
maji ya visima na kuahidi ikiwa atashinda atahakikisha kunachimbwa
visima vyenye maji matamu na kuweka mtandao wa usambazaji maji katika
kila nyumba kwenye jimbo hilo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment