Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ametoa kauli ambayo bila shaka imewagusa wengi katika jamii.
Akinukuliwa na gazeti hili juzi alipokuwa
akifungua Chuo cha Ualimu cha Benjamin Mkapa kilichopo Wilaya ya Wete
kisiwani Pemba, Mzee Mkapa alitoa rai kwa Serikali iliyopo madarakani
kuboresha masilahi ya walimu, jambo alilosema alishindwa kulitekeleza
wakati wa utawala wake.
Japo amekiri kuwa masilahi ya walimu bado yapo
chini na kwamba alifanya makosa kutowasaidia, huku akishauri utawala wa
sasa kutoiga makosa yaliyofanywa na uongozi wake, sisi tunasema kauli
hiyo ni ya mtu anayejikosha.
Katika nchi hii, walimu kama kada muhimu na nyeti
kwa Taifa, wamekuwa wakiilalamikia Serikali kutowapa haki na stahili zao
mbalimbali kwa miaka nenda rudi.
Kinachosikitisha ni kuwa badala ya kuzivalia njuga
kero za walimu, Serikali karibu zote zimekuwa zikitumia nguvu za dola
kufifisha harakati na juhudi za walimu kudai haki zao. Serikali zetu
zimekuwa zikifanya mazungumzo ya mara kwa mara na baadhi ya kada za
utumishi na hata kutekeleza ahadi inazotoa ili kupoza watumishi wake,
lakini zimeshindwa kufanya hivyo kwa walimu.
Matokeo yake, walimu wanaendelea kuumia. Ukitoa
udogo wa mishahara yao na kutolipwa hata zile stahili zao halali,
mazingira ya kazi vituoni nayo yanazidi kuongeza ukubwa wa tatizo.
Tunaamini baadhi ya kero sugu za walimu kama vile
malimbikizo ya mishahara kwa wanaopanda madaraja, malipo ya fedha za
likizo na uhamisho zimo ndani ya uwezo wa Serikali ya sasa na hata
iliyopita chini ya Mkapa.
Kama rasilimali za nchi zitagawanywa kwa haki na
kufuata vipaumbele muhimu vya taifa, huku mianya ikizibwa ili watu
wachache wasitapanye rasilimali hizo au kujinufaisha wao binafsi,
Serikali zetu zina uwezo mkubwa wa kumaliza kero hizi.
Kinachoonekana ni kuwa Serikali hazijawa na azma
madhubuti ya kumaliza kero hizi na nyinginezo zinazowakabili walimu wa
Tanzania.
Kukiri makosa yanayoweza kuepukwa hakusaidii kumaliza vilio vya walimu au hata kukuza hadhi ya ualimu ambayo sasa imeshapotea.
Uzoefu unaonyesha viongozi wastaafu nchini
wameanza kujenga tabia ya kukemea, kuelekeza na hata kuwakosoa wenzao
pale wanapotoka madarakani. Mathalani wapo wanaokemea vitendo vya rushwa
na ubadhirifu serikalini ilhali walishindwa kufanya hivyo walipokuwa
madarakani tena katika nyadhifa kubwa.
Kama awamu ya tatu licha ya kutambua haja ya
kuboresha masilahi ya walimu, ilishindwa kuwatimizia haja zao, hii
inabaki kuwa changamoto kwa utawala wa sasa ili viongozi wake wasije
kuendeleza ada iliyoanza kujengeka ya viongozi wastaafu kutoa udhuru wa
kushindwa kutekeleza majukumu wakiwa nje ya ulingo wa uongozi.
Awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imebakiwa na miaka
miwili kumaliza muhula wake. Vilio vya walimu vinaendelea, hadhi na
heshima ya walimu na ualimu vimeshaporomoka siku nyingi. Rais na timu
yake bado wana nafasi ya kurekebisha hali ya mambo.
Serikali yetu isijitue mzigo wa kero za kimasilahi
na mazingira ya ufanyaji kazi zinazowakabili walimu nchini. Serikali
ndio mwajiri wa walimu na mtatuzi wa mambo yanayowasibu.
Walimu ni nguzo na chachu ya maendeleo ya Taifa
hili. Wataalamu na watendaji wanaotarajiwa kuiletea maendeleo nchi
lazima wapitie mikononi mwa walimu. Kwa kuzingatia umuhimu wao, Serikali
haina budi kuwajali walimu hasa kwa kuwatimizia masilahi yao.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment