SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar ipo mbioni kuleta meli kubwa na ya
kisasa itakayokuwa ikisafirisha abiria kutoka Unguja kwenda Pemba
ambayo itakuwa na garantii ya usalama.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali
Vuai, alitoa kauli hiyo mjini Unguja juzi alipohutubia mkutano wa tano
wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki
uliofanyika viwanja vya Kisima mbaazi, Kiembesamaki.
Akimnadi mgombea nafasi ya uwakilishi wa jimbo hilo kupitia CCM,
Mahmoud Thabit Kombo, aliwataka wananchi kukiunga mkono chama hicho ili
kuendelea kuwaletea maendeleo na kuimarisha Muungano ambao sasa
unadumu kwa miaka zaidi ya 50.
Alisema katika kuzingatia sera, ilani na kanuni za chama, tayari
serikali imeshaagiza meli kubwa na ya kisasa ambayo itakuwa ikichukua
abiria wengi na kwa wakati katika kufanya safari zake Unguja na Pemba.
“Meli ipo njiani, na itawasili muda wowote kuanzia sasa. Itakuwa
mkombozi kwa wananchi wa visiwa hivi ambapo watapata chombo chenye
garantii katika usafiri wa majini,” alisema Vuai.
Mgombea wa uwakilishi wa jimbo hilo, Mahmoud Thabit Kombo, alipongeza
wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo na kuwaomba kumpa
kura za ndiyo kwenye uchaguzi utakaofanyika Februari 2.
Mahmoud alisema atahakikisha anasimamia sera na Ilani ya CCM katika
kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuwatetea wananchi kwenye Baraza
la Wawakilishi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment