WAKATI viongozi wakuu wa serikali wakiwa katika mchakato wa kuteua
wabunge 201 wa Bunge la Katiba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi,
Yussuf Mohamed Yussuf, amesema mfumo wa serikali tatu kama utapitishwa
uhai wa muungano utabaki shakani.
Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa, alibainisha hayo jana kwenye mkutano wa
hadhara wa kampeni za Jimbo la Kiembesamaki uliofanyika uwanja wa
Garden mjini Unguja wakati akimdadi mgombea wa chama hicho, Mahmoud
Thabit Kombo.
Alisema maisha ya Watanganyika na Wazanzibari yanategemeana kulingana
na miingiliano ya kihistoria na mlingano wa maisha ukifanana na
mabadiliko ya mfumo na ujio wa serikali tatu huenda ukawa hatari na
balaa jipya nchini.
Alisema watu waliotoa maoni ya kutaka muungano wa mkataba hawakufikia
malengo yao na kwamba pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
linalotaka mfumo wa serikali tatu lisishangiliwe kama ushabiki wa
Simba na Yanga.
“Wananchi msikubali kupelekwa puta, CCM haitapepesa macho wala
masikio yake kuafiki mfumo mpya, tunajua una hatari na majanga,
watakaopata shida ni wananchi wanyonge, zitazameni adha zilizopo hivi
sasa Libya, Syria, Sudan Kusini, ” alisema.
Alieleza kutokana na vyanzo haba vya kiuchumi vilivyopo Zanzibar,
serikali ya tatu itakuwa ni vigumu kuigharamia na kwamba ukitaka kujua
Zanzibar inaitegemea Tanzania Bara kiuchumi aliwataka wakaangalie
wasafiri katika bandari ya Malindi kutoka Bara wakibeba vikapu vya
mchele, mbatata na nyanya kutoka Tanganyika.
Aidha, mwenykiti huyo wa CCM aliwataka wananchi kutowasikiliza
viongozi wa CUF akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, wanaoshabikia
mabadiliko ya mfumo huo kwa kufikiria kushika madaraka na masilahi
binafsi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment