Home »
» CCM Z'bar: kauli ya CUF inasikitisha
CCM Z'bar: kauli ya CUF inasikitisha
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimedai kimesikitishwa na kauli za
uchochezi zilizotolewa na Chama cha Wananchi (CUF), kuhusu uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki, uliofanyika Februari 2 mwaka huu,
visiwani humo.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa
Zanzibar kutoka Idara ya Oganaizesheni, Bw. Haji Mkema Haji, aliyasema
hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema kitendo cha
CUF kudai uchaguzi huo haukuwa huru na haki, kinaonesha chama hicho
hakijakomaa kisiasa ambapo kauli hiyo, haileti taswira nzuri kwa
Zanzibar.
"CCM imesikitishwa na taarifa hii ya uchochezi, upotoshaji
mkubwa kwa jamii iliyotolewa na viongozi wa CUF kwa waandishi wa
habari," alisema Bw. Haji.
Aliongeza kuwa, jimbo hilo ni ngome ya
CCM na si mara ya kwanza kwa CUF kulalamika na kutoa madai kama hayo
jambo ambalo linaonesha hawajakomaa kisiasa.
Bw. Haji alisema chama
chao kimeridhishwa na uchaguzi huo pamoja na kuwapongeza wakazi wa jimbo
hilo kwa kumchagua Bw. Mahmoud Thabit Kombo kushinda kuwa mwakilishi
wao.
Alisema hawakutarajia kusikia kauli kama hizo hasa wakati huu
ambao Zanzibar ipo katika muundo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa ili
kumaliza siasa za chuki, uhasama na uzushi.
Aliwataka viongozi wa
CUF kuacha kutoa malalamiko yasiyo na maana kwani kufanya hivyo ni
kurudisha siasa za chuki ambazo hivi sasa hazina nafasi tena.
Wiki
iliyopita, CUF ilimuomba Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kuifuta Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), na kudai imeshindwa kusimamia vyema chaguzi mbalimbali
visiwani humo.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Haki za Binadamu na
Mawasiliano ya Umma wa CUF Zanzibar, Bw. Salim Bimani alisema chama
hicho hakijaridhishwa na mwenendo wa ZEC ambayo imekuwa ikishindwa
kuendesha chaguzi kwa misingi ya haki na uhuru.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment