RAIS
wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewaambia wafanyabiashara wa
viungo mjini Mumbai, kuwa Zanzibar haina pingamizi kuwauzia karafuu zake
moja kwa moja na akawataka wafanye mazungumzo na Shirika la Biashara la
Zanzibar-BI ZANJE kuhusu jambo hilo.
Rais alikutana na
wafanyabiashara hao baada ya kutembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza
viungo cha Everest, kilichoko nje kidogo ya jiji la Mumbai.
Aliwaeleza
wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa
inatekeleza mkakati wa kufufua zao la karafuu ambalo lilidumaa miaka
iliyopita.
Alisema mkakati huo ambao unajumuisha kuongeza kasi ya
upandaji wa mikarafuu mipya pamoja na kuwapa wakulima bei nzuri ya soko,
uzalishaji umeanza kuongezeka na hata kuweza kutosheleza mahitaji ya
wafanyabiashara hao ambayo tani 10,000 kwa mwaka.
Dkt. Shein alitoa mwaliko rasmi kwa wafanyabiashara hao kutembelea Zanzibar na kufanya mazungumzo na Shirika la ZSTC.
Awali,
baadhi ya wafanyabiashara hao walieleza changamoto zilizowafanya kuacha
kununua karafuu moja kwa moja kutoka Zanzibar kwa hiyo tamko hilo la
Rais wa Zanzibar walieleza kuwa limewatia moyo na kuahidi kufanya
biashara hiyo moja kwa moja na Zanzibar .
Walibainisha kuwa wao
wanazihitaji sana karafuu za Zanzibar kutokana na ubora wake na
kuzisifia kwa kusema kuwa ndiyo 'Mfalme wa karafuu duniani'.
Akizungumzia
historia ya biashara kati ya Zanzibar na India, Dkt.Shein alisema
biashara kati ya nchi hizo imedumu kwa miaka karibu 150 na kwamba
Zanzibar ipo tayari kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano na
Kampuni ya viungo ya Everest ambayo inatumia karafuu na viungo vingine
kwa wingi.
Wakati huo huo, Dkt. Shein amesema ziara yake nchini humu
imekuwa ya mafanikio na kufikia malengo yake.Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kutembelea kiwanda cha kusindika viungo mjini hapa
jana Dkt. Shein aliwaeleza waandishi hao kuwa ziara yake hiyo imepata
mafanikio katika kuimarishau husiano wa kidiplomasia na kisiasa kati ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya India.
Kwa upande
mwingine alifafanua kuwa ziara hiyo ya siku tisa iliyomuwezesha kuzuru
miji ya New Delhi, Jaipur, Hyderabad, Bangaluru na Mumbai imeiwezesha
Zanzibar na India kuimarisha ushirikiano katika sekta za utalii,
uwekezaji, afya, kilimo na uwezeshaji wananchi.
Aliongeza kuwa mbali
ya kutia saini makubalinao ya ushirikiano katika baadhi ya sekta lakini
pia wahusika wa sekta hizo wamealikwa kutembelea Zanzibar kwa
mashauriano zaidi katika kuendeleza ushirikiano katika sekta zao.
Dkt.
Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa India hususan Makamu
wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Mohammad Hamid Ansari na Waziri Mkuu Manmohan
Singh kwa kumualika kuzuru India rasmi.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment