Home » » Shehena ya magogo yanaswa

Shehena ya magogo yanaswa

Makontena sita yaliyobeba magogo yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nje kwa njia za magendo yamekamatwa katika Bandari ya Malindi, Kisiwani Unguja kabla ya kusafirishwa kuelekea nchini China, imefahamika visiwani humu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Operesheni ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) Kanda ya Zanzibar, Ali Bakari amethibitisha makontena hayo kuzuiwa. Uchunguzi umeanza kufanyika baada ya kubainika kuwa yamesafirishwa kinyume na sheria yakitokea nchini Madagascar.
Bakari alisema chimbuko la kukamatwa kwa makontena hayo kumetokana na taarifa zilizotolewa na Shirikisho la Huduma za Forodha Duniani, (WCO) kwamba kuna meli zinazobeba magogo kutoka Madagascar na kupitishwa katika mwambo wa Tanzania na Kenya.
Meneja huyo alisema taarifa hizo zilieleza kuwa matukio hayo yangetokea kati ya Agosti na Februari mwaka jana na mwaka huu katika mwambao wa Tanzania. Baada ya kuanza kufuatilia ikabainika kuanza kujitokeza kwa meli ndogo ndogo zikishusha magogo Visiwani Zanzibar.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja jina la kampuni inayomiliki magogo hayo na kuitumia Kampuni ya Wakala wa Mizigo ya Visiwani Enterprises kusafirisha mzigo huo .
Kuhusu sakata hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Maliasili, Sheha Idrisa Hamdan alithibitisha kuingizwa kwa shehena ya magogo Zanzibar zikitokea Madagascar.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa