KAMPUNI ya (C. WEED COOPORATION) tawi la Pemba, imetoa msaada wa vifaa wa kilimo cha mwani wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50/= kwa wakulima wa mwani katika shehia tofauti Kisiwani humo.
Akitoa msaada huo kwa nyakati tofauti kwa vituo mbali mbali vya kununulia mwani, Meneja wa kampuni hiyo tawi la Pemba, Nd.Jabir Salim Chamshama, amehimiza ugaiwaji wa kamba hizo kwa wakulima, ili ziweze kufanyiwa kazi na kufikia malengo yaliokusudiwa na kampuni.
Katika maelezo yake, Chamshama amesema kuwa lengo hasa la kugawa zana kwa wakulima ni kusaidia wananchi walio katika hali za chini kimaisha, kumudu gharama kutokana na ukali wa maisha na kuongeza uzalishaji katika zao la mwani Visiwani Zanzibar.
Akizungumzia suala la bei, amewataka wakulima hao kuwa wastahamilivu kutokana na soko la dunia kutoamua kuwapandishia bei, huku wakiongeza bidii katika uzalishaji kwa kulima mwani wenye bei pamoja kuukausha vyema na kuacha tabia ya kuuweka na takataka jambo ambalo linapunguza thamani na hadhi ya mwani.
Kwa upande wake, bwana shamba kutoka kampuni ya (C. WEED COOPORATION), Mohamed Hassan Nassor, amewataka wakuu wa vituo vya kununulia mwani, kuwapatia elimu wakulima wa zao la mwani juu ya gharama ambazo zinatumika kununulia vifaa, ili kuondosha dhana potofu baina yao na makampuni.
Hata hivyo amewataka wakulima kuzitumia kamba hizo kwa malengo yaliokusudiwa, ili kuongeza uzalishaji na kuepuka kuzirundika ndani na kuzitumia kinyume cha malengo ya kampuni.
.
Aidha amewashauri wakulima, kuwa waaminifu kwa makampuni wanayokubaliana na kupatiwa vifaa kwa lengo la kuwauzia mwani, pamoja na kulima mwani wa ‘Cottonii’ (mwani mnene) ambao unahitajika zaidi na bei yake ni nzuri katika soko la dunia.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment