Home » » WAZANZIBARI WAJIPANGA KUTAKA MGAO ZAIDI

WAZANZIBARI WAJIPANGA KUTAKA MGAO ZAIDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar wamejipanga ili kuwashawishi wajumbe wengine wakubali pendekezo la kuiongezea Zanzibar, mgawo wa mapato ya Muungano.
Mmoja wa wajumbe hao, Juma Ali Khatibu alisema Zanzibar inapaswa kuongezewa mgawo kutoka asilimia 4.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 20.
“Zanzibar tulisema kuwa hatunufaiki na ajira za Serikali ya Muungano lakini hilo limetatuliwa na sasa tunataka tuongezewe mgawo wa mapato,” alisema Khatibu.
Akimnukuu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, Khatibu alisema Wazanzibari wanapata asilimia 21 ya ajira kwenye taasisi za Muungano.
“Kwa hiyo kupitia Bunge hili, mimi nilikuwa nawaomba Wazanzibari wenzangu tuitetee Zanzibar hasa kwenye ile asilimia 4.5 ya mgawanyo wa mapato,” alisema.
“Wakati ule tulikuwa 300,000, siku hizi tumekuwa wengi. Hapa ndiyo mahali pa kuomba mgawo uongezeke kutoka asilimia 4.5 hadi angalau 20 au 21 hivi,” alisisitiza.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood, ambaye alisema mgawanyo wa mapato ya Muungano ni jambo linalopaswa kuzungumzwa kwa kina.
“Ni jambo kubwa sana linalohitaji kuzungumzwa kwa kina katika Bunge letu hili. Ukiondoa tatizo hili manung’uniko yote yatakuwa yamekwisha,” alisema Abood.
Abood ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo, alisema kimeanzishwa chombo cha kusimamia masuala ya fedha kwa pande mbili za Muungano.
“Wazanzibari wapate fursa iliyo sawa na Bara. Tutengeneze msingi utakaotengeneza usawa katika mgawanyo wa mapato,” alisisitiza.
Waziri huyo alisema suala la Zanzibar kuongezewa kiwango cha mgawo linazungumzika katika Bunge Maalumu la Katiba, kama kutakuwa na dhamira njema.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa