Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Masoud
Othman Masoud amesema hajawahi kuuona waraka ulioandikwa na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar (BLW) na kusainiwa na Spika Pandu Ameir Kificho
unaopendekeza Tanganyika na Zanzibar kuwa na mamlaka huru za dola na
kuwasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza na Mwananchi AG Masoud amesema waraka
huo ulitayarishwa na kamati ya uongozi chini ya Mwenyekiti wa kamati
hiyo Spika Kificho, baada ya kufanyika vikao vilivyowahusisha wajumbe wa
kamati ya uongozi ya Baraza hilo na kutoa mapendekezo yake.
Masoud alisema licha yeye kuwa si mjumbe wa kamati
hiyo lakini huingia kama mjumbe mualikwa, ambapo kikao cha kwanza
alishiriki kujadili mambo ya msingi yanayotakiwa kuwasilishwa katika
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama maoni ya taasisi lakini hakumbuki
kuhudhuria kikao cha mwisho ambacho kiliandaa mapendekezo hayo.
“Mpaka sasa waraka uliowasilishwa mbele ya Tume ya
Jaji Warioba bado sijauona kwa macho yangu, siwezi kusema kama ulikuwa
waraka halali au batili ila nasikia mivutano inayojitokeza miongoni mwa
wajumbe wake,” alisema AG Masoud.
Alisema Baraza kama Taasisi lilitoa maoni kama
walivyotoa maoni baadhi ya makatibu wakuu wa SMZ na taasisi nyingine
ambazo zinaguswa au kufanya kazi zinazohusiana na mambo ya msingi
yaliomo katika orodha ya mambo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Aidha, alisema kama kamati ya uongozi ya Baraza
akidi ya wajumbe ikitimia ina uwezo wa kutoa mapendekezo kwa niaba ya
taasisi na kusema si mwafaka kwa sasa kumjadili Spika peke yake, kama
kuna ukiukwaji wa sheria au kanuni za Baraza kulikojitokeza.
Pia Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ alibeza kitendo
cha Baraza la Wazee wa CCM kuondoa imani kwa Spika Kificho na kumtaka
ajiuzulu, badala yake alisema kama kuna makosa yamefanyika, basi kamati
nzima ya uongozi ya Baraza hilo inatakiwa ijiuzulu.
“Si haki na sahihi kumshinikiza Spika ajiuzulu,
kama kuna kasoro zimefanyika, kamati nzima ya uongozi ya BLW nayo
inapaswa kuwajibika. Suala hilo halikuwa la Spika ila ni la taasisi,”
alisema Mwanashseria Mkuu huyo wa SMZ.
Alisema kimsingi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
haina maoni wala mapendekezo yake kuhusu mabadiliko ya muundo wa
Muungano uweje na hata Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, hajawahi
kuweka bayana msimamo wake kama kiongozi Mkuu wa Zanzibar.
Hata hivyo AG Masoud alikiri kuwa msimamo pekee
ambao Dk Shein amekuwa akiutetea ni ule wa chama chake wa kuendelea
kuwapo muundo wa Muungano wa Serikali mbili ambao hautokani na msimamo
wa SMZ.
Mwanasheria Mkuu huyo pia alisema ni mapema kwake
kutoa tathmini na mwelekeo wa mjadala wa Bunge la Katiba kama Zanzibar
itaweza kufikia malengo yake ya kupata katiba yenye masilahi na
Zanzibar, kutokana na mgawanyiko uliopo wa wajumbe kutoka Zanzibar
uliojitokeza unaoegemea sera za vyama na itikadi za kisiasa.
Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar tayari limetoa tamko la kupoteza imani na Spika Kificho kwa
kitendo chake cha kuandika waraka unaopendekeza Zanzibar na Tanganyika
zipate mamlaka huru za dola, bila ya kuwepo kwa mapatano na uamuzi wa
pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Wazee hao wamesema hiyo ni aina ya hujuma na usaliti kinyume na
utaratibu wa hadhi ya Spika aliyekabidhiwa dhamana hiyo nyeti katika
mgawanyo wa madaraka chini ya mihimili mitatu.
Kwa upande wake Spika Kificho amekiri kuwa hakuna
uamuzi wa pamoja uliofikiwa na Baraza lake katika kupendekeza aina ya
muundo wa mfumo wa Muungano, kutokana na pande mbili za kisiasa za CCM
na CUF kila moja kuwa na msimamo wake kisera.
Kificho ameendelea kusisitiza kuwa waraka
aliousaini na kuuwasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji
Joseph Warioba, ulijadiliwa na kuridhiwa na kamati ya uongozi jambo
ambalo limekanushwa na Mnadhimu wa Baraza hilo upande wa CCM, Salmin
Awadh Salmin ambaye alisema waliotoa mapendekezo hayo ni kigenge cha
watu watano kinyume na utaratibu wa pamoja wa kamati ya uongozi yenye
wajumbe 15.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment