Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Bunge la Katiba limeanza kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya
Katiba katika sura ya kwanza na sura ya sita ambayo kwa kiasi kikubwa
inahusu Muundo wa Muungano.
Sura hizi mbili, ndizo ambazo zinaelezwa kuwa ni
roho ya mjadala wa Katiba katika Bunge hilo Maalumu kwa kuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, imependekeza Muundo wa Muungano wa serikali tatu
katika sura hizo na ibara nyingi katika rasimu inayojadiliwa, zinajengwa
kwa muundo huo wa Muungano.
Wakati akiwasilisha Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba
bungeni Jaji, Joseph Warioba alitoa sababu nyingi za tume kufikia
kukubali mapendekezo ya wananchi kuhusu serikali tatu.
Miongoni mwa sababu kubwa ni pamoja na sasa
Muungano kubadilika kuwa ni wa serikali mbili na nchi mbili, Muungano
ambao siyo ule ulioachwa na waasisi Hayati Julius Nyerere na Abeid
Karume wa serikali mbili nchi moja.
Nchi mbili ndani ya Muungano, zimetokana na
Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, ambayo
yalifanyika mwaka 2010.
Katika mabadiliko hayo yaliyopo katika sehemu ya
kwanza tu ya Katiba ya Zanzibar yanasema Zanzibar ni nchi ambayo eneo la
mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja visiwa
vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambavyo kabla ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.
Zanzibar ni sehemu ya Muungano
Namba mbili katika katiba hiyo sehemu ya kwanza,
inaeleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zilizounda Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Sehemu ya pili(a) inaeleza kuwa , kwa ajili ya
utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais anaweza kuigawa Zanzibar
katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa
na sheria iliyototungwa na Baraza la Wawakilishi.
Katiba ya Zanzibar pia imebadili masharti ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema Sheria za Muungano zinazotungwa
na Bunge la Jamhuri, zitume sehemu zote, lakini kwa sasa Zanzibar ili
Sheria ya Muungano itumike ni lazima ipelekwe Baraza la Wawakilishi.
“Maana yake ni kuwa, Katiba ya Zanzibar ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” anasema Jaji Warioba.
Kutokana na utata huu, Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hamad Yusuph Masauni alifanya mahojiano na gazeti hili na kueleza ifuatavyo;
Swali: mababadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010,
yanatajwa kuwa moja ya mambo ambayo yamechangia sana mapendekezo ya
Serikali tatu, je nini maoni yako?
Jibu: Ni kweli kuwa yamefanyika mabadiliko hayo,
lakini kwa ufahamu wangu mimi nadhani Zanzibar hawajavunja Katiba, kwani
kusema tu Zanzibar pia Katiba ya Zanzibar kumpa Mamlaka Rais kuigawa
katika mikoa na wilaya siyo kosa.
Swali: lakini jambo hili linatajwa kuwa nyeti
kwani kwa kiasi kikubwa licha ya matatizo mengine, inaonekana ndilo
limebariki uwepo wa serikali tatu.
Jibu: Hapana. Kwanza naomba ieleweke Suala la
Tawala za mikoa siyo la Muungano hivyo, haimzuii Rais wa Zanzibar kugawa
mikoa na wilaya kwani jambo hili si la Muungano.
Swali: Unadhani ni kwa nini Zanzibar imefikia kufanya mabadiliko haya makubwa ya Katiba yake?
Jibu: Mimi sioni kama kuna tatizo, lakini kwa kuwa
sasa tunatengeneza Katiba ya Muungano ni vyema tukafanya marekebisho
kama tunataka kulifanya suala la tawala wa mikoa liwe la Muungano.
Swali: Masauni wewe ni mbunge wa Jamhuri wa Jimbo
la Kikwajuni Zanzibar. Hivi sasa kuna mjadala mzito juu ya Muundo wa
Serikali nini maoni yako?
Jibu: Mimi naunga mkono msimamo wa chama changu na wananchi wa jimbo langu kuendelea na muundo wa serikali mbili.
Swali: Lakini muundo huu unaonekana kulalamikiwa
na Wazanzibari wengi kutokana na hoja kuwa Tanganyika imevaa koti ya
Muungano na fedha nyingi zinaendesha Maendeleo ya Tanganyika badala ya
Zanzibar.
Jibu: Ni kweli kuna madai hayo, lakini naamini
changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi kama ambavyo aliahidi Rais Jakaya
Kikwete alipokuja kuzindua bunge.
Swali: Lakini hata baada ya bunge kuzinduliwa na
kutolewa ahadi hizo na Rais Wazanzibari na hata wanaounga mkono mfumo wa
Serikali tatu, wanasema hata katika bunge hilo bado kunaonyesha
Zanzibar kumezwa. Nini Maoni yako?
Jibu: Hayo ni madai ya wanasiasa wachache ambao
wana malengo ya kushika dola kama mfumo wa Serikali tatu, ukipita lakini
mimi binafsi naamini Zanzibar haijamezwa bungeni kwanza katika kamati
zote kama Mzanzibari siyo mwenyekiti basi ni makamu.
Swali: Je, wewe binafsi kwa mtazamo wako unaona ni Muundo wa
Serikali ngapi unafaa na je, wananchi wa jimbo lako watakuelewa kwa
kutetea msimamo wa chama chako?
Jibu: Mimi naunga mkono serikali mbili na hakika
nikirudi na serikali tatu wananchi wangu hawatakubali sio kwa sababu
jimbo langu wana ccm ni wengi lakini wana hoja.
Swali: Baraza la Wawakilishi limetajwa pia
kupendekeza muundo wa serikali tatu, hasa kutokana na hoja yao, kutaka
Zanzibar yenye Mamlaka, Tanganyika yenye Mamlaka na kujulikana Mamlaka
ya Muungano.
Jibu:Binafsi siwezi kuzungumzia maoni ya wawakilishi lakini nadhani tatizo ni tafsiri tu zinachanganya watu.
Swali: Unadhani sasa Bunge hili la Katiba linaweza
kusaidia kuondoa matatizo ya Zanzibar na hata Tanganyika katika mfumo
wa Muungano uliopo?
Jibu: Ndio kwani Bunge hili lina jukumu kubwa la
kutunga sheria ambazo ndizo zitakuwa kuu kwa pande zote na kuondoa kero
za muda mrefu kwa kila upande.
Swali: Nini hofu yako katika Muundo wa serikali tatu?
Jibu: Hakuhitaji mtu kuwa ya PhD kujua kuwa
serikali tatu zitaua muungano wetu, hofu yangu mimi bila Serikali mbili
muungano unakwenda kufa.
Swali: Nini maoni yako ya jumla kuhusu Bunge Maalumu la Katiba?
Jibu: Mimi wito wangu kwa wajumbe,tutengeneze
Katiba hii kwa maslahi ya wananchi na sio masilahi yetu. Hakuna wananchi
ambao wanataka vurugu zitokee katika Bunge hili hata baada ya
kupitishwa mapendekezo ya Katiba.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment