Home » » THELUTHI MBILI YAGOMA KURA WAJUMBE ZANZIBAR

THELUTHI MBILI YAGOMA KURA WAJUMBE ZANZIBAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

  Wajumbe wa Bara zaelezwa kutimia
  Kura mseto zadaiwa kutafuna muda
Mwenyekiti wa Kamati Na.8 ya Bunge Maalum la Katiba, Job Ndugai.
 
Wakati  mfumo wa upigaji kura mseto yaani za siri na wazi ukidaiwa kuzorotesha kasi ya maamuzi ndani ya Kamati za Bunge Maalum za Katiba, upatikanaji wa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar katika kupitisha baadhi ya ibara unaelezwa kuwa mgumu.
Hali hiyo imeelezwa kutokea katika kamati walau tatu kati ya 12 ambazo zimekwisha kupiga kura ambazo ni namba moja, nane na 10.

 Mwenyekiti wa Kamati Na. 8 ya Bunge Maalum la Katiba, Job Ndugai, alisema kuwa utaratibu huo ni mgumu kutekelezeka na unachukua muda mrefu kutokana kila kifungu kutakiwa kupigiwa kura ili kukipitisha.

Alisema pia sharti la kupata theluthi mbili ya kila upande kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ni kikwazo kingine kwa kamati yake kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba kwa kasi inayotakiwa kutokana na wajumbe kutokubaliana, hivyo kufanya idadi ya wajumbe inayotakiwa kwa mujibu wa kanuni kushindwa kutimia.

“Changamoto kubwa inayotukabili ni suala zima la muda kwani utaratibu huu wa kupiga kura ya siri na wazi kwa wakati mmoja unachukua muda mrefu kiasi kwamba kuutumia katika kila kifungu tunaweza kuchukua zaidi ya siku mbili, katika hali hiyo inapotokea akidi ya theluthi mbili kutoka kila upande inakosekana, mambo yanakuwa magumu zaidi,” alisema Ndugai.

Alisema kuwa kutokana na ugumu huo, kamati yake inatarajia kuomba muda zaidi wa kuendelea kujadili sura mbili za Rasimu zinazojadiliwa na kamati zote ili iweze kukamilisha kazi hiyo kwa ufasaha na kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalum la Katiba.

“Kwa muda tuliopewa pamoja na nyongeza ya siku ya leo (jana), bado muda hautoshi, hivyo tunakusudia kesho (leo) kuomba Bunge Maalum la Katiba kutuongeza muda ili tuweze kukamilisha kazi yetu,” alisema Ndugai.

Akizungumzia kuhusiana na namna mjadala ulivyokwenda ndani ya kamati yake, Ndugai alisema ulikuwa ni mkali na kuwa wajumbe walikuwa wakitofautiana kimawazo katika baadhi ya maeneo, ingawa hakuna lugha za matusi, vijembe wala mivutano iliyojitokeza wakati wa majadiliano hayo.

Hata hivyo, alisema yapo baadhi ya mambo ambayo wajumbe walishindwa kuyaelewa na ikawalazimu kumwita aliyekuwa Katibu wa Bunge wakati Tanganyika na Zanzibar zikiungana, Pius Msekwa, kwa ajili ya kutoa ufafanuzi.

Alisema baada ya Msekwa kutolea ufafanuzi baadhi ya mambo, wajumbe wote waliridhika na kuendelea na kikao kama kawaida.

Hata hivyo, Ndugai alipotakiwa kueleza kama katika kamati yake pia uliibuka utata juu ya hati ya Muungano, alithibitisha kutokea mvutano na kusema kuwa ndiyo sababu kubwa ya kuitwa kwa Msekwa na kuhojiwa.

Alisema mbali na hati ya Muungano, wajumbe walipitia nyaraka nyingine zilizopo na kujiridhisha, kisha wakaendelea kujadili mada iliyokuwa mezani.

KAMATI NA. 11

Wajumbe katika baadhi ya kamati wameonyesha kutaka Muungano uendelee, lakini wanatofautiana kwenye muundo wa serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kuhusu majadiliano ya Sura ya Kwanza na ya Sita kwenye Kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati Na. 11, Anne Kilango Malecela, alisema wajumbe wa Tanzania Bara na Visiwani wote wanautaka Muungano.

Alisema katika kamati yake hakuna aliyesimama akasema hataki Muungano.

“Wajumbe wote 54 wanataka Muungano, tatizo wanatofautiana kwenye muundo, wapo wanaotaka Muungano wa Serikali tatu na Muungano wa serikali mbili,” alisema.

Alisema kamati yake imeshapitia sura ya kwanza na sita na kufanyiwa marekebisho, na walitarajia kuanza kupiga kura ya kupitisha mabadiliko hayo jana jioni.
 
KAMATI NA. 10
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Na. 10, Anna Abdallah, alisema katika baadhi ya mambo, Bara na Visiwani wametofautiana.

Wajumbe wa Zanzibar ni 15 na theluthi mbili yao ni 10, na upande wa Bara ni 37, na theluthi mbili yao ni 25.

Alisema wakati mwingine kuna masuala ambayo upande wa Zanzibar wanakubaliana na upande wa Bara na kupata kura zote za ndiyo, lakini wakati mwingine wanagawanyika katika misingi ya vyama na itikadi.

“Kwa kuwa sura ya kwanza na ya sita zinashabihiana, tumefanya msingi kwa mfano  unaposema shirikisho inatafsiri kabisa kuwa lile shirikisho ni la serikali tatu,” alisema.
Alisema katika Muundo wa Serikali tatu au mbili, walio wengi kwenye kamati hiyo wamesema serikali mbili.

“Tatizo liko kwenye muundo wa serikali mbili, au tuwe kwenye shirikisho la serikali tatu. Hapo kila tukipiga kura tunapata theluthi mbili, lakini Zanzibar hatupati theluthi mbili,” alisema.

Alisema wamekubaliana kuwa tangu mwanzo  kupiga kura kwa maneno hayo ya shirikisho ama Muungano wa Serikali mbili. Aliongeza kuwa hayo hayasumbui tena katika mjadala wao.

“Taarifa yetu itakuwa wengi wamesema muundo wa serikali mbili, pamoja na sababu zake. Na kutakuwa na taarifa ya wachache wanaosema shirikisho la muundo wa serikali tatu ndilo linalofaa,” alisema.

Alisema kila mjumbe aliyetakiwa kufanya mabadiliko kwenye vifungu, aliambiwa akaandike kwenye karatasi na baadaye yalichapwa na kila mjumbe alipata nakala. Kila mjumbe alipata nafasi ya kuelezea mabadiliko yake kwa dakika tatu.

Aliongeza kuwa hakuna matatizo ya wajumbe kutoelewana, utulivu ulikuwa mkubwa ndani ya kamati na wajumbe walikuwa wanaambiana ukweli.

“Muda wa kujadili ulikuwa mdogo ili kupata nafasi ya kuhakikisha kwamba yaliyoandikwa neno kwa neno, para kwa para yana maudhui na yaliyoandikwa kwenye sura nyingine hayakinzani na sura nyingine, hiyo inakuwa ni kazi kidogo,” alisema.

 “Utashi wa kutaka kuchangia na kuboresha upo kwa wajumbe wa kamati yangu,” alisema.

 “Tumekubaliana mambo ya msingi, kwa mfano tumepiga kura kuhusu mipaka ya Muungano kwa vyovyote pale palikuwa pamekosekana mito, maziwa, milima. Sisi tuliongeza milima na anga na wote tulikubaliana.”
 
KAMATI NA. 1
Wajumbe wengi ndani ya kamati hiyo walitaka ibara inayohusu shirikisho katika sura ya kwanza ibara ya kwanza iondolewe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ummy Mwalimu, alisema mvutano mkubwa uliopo kwenye kamati hiyo ni kuhusu shirikisho na kuwa wajumbe wengi wanataka neno hilo liondolewe. 

Ibara 1(1) inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye Mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.

Alisema wajumbe wengi katika kamati hiyo walitaka neno hilo la shirikisho liondoke na kubaki neno Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi yenye Mamlaka Kamili.

“Sasa kuna wajumbe wengine wakawa wanataka ile ibara ibaki kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba…kwa hiyo ilikuwa mvutano na ndiyo ikapelekea sasa watu kudai Hati ya Makubaliano ya Muungano,” alisema.

Alisema kamati hiyo jana ilianza kwa kupigia kura sura ya kwanza ya Rasimu ya Katiba baada ya kukamilisha mjadala ambao ulijikita katika sura hiyo ambayo inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho.

“Hapa tulipoteza siku ya kwanza yote kwa ajili ya kujadiliana…wajumbe walikuja na hoja, vielelezo na maandiko na wame-quote (nukuu) maprofesa kwa kweli mjadala ulikuwa umetulia,” alisema.

Mwalimu alisema jana mchana walitarajia kuanza mjadala wa sura ya sita ya Rasimu hiyo ambayo inazungumzia Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Leo (jana) tukaendelea kufanya maamuzi ya ibara nyingine za sura ya kwanza…na tumeshafanya maamuzi…wangapi wanataka nini…maoni ya wengi na wachache yakoje, yatawekwa kwenye taarifa ya kamati ambayo yatawasilishwa ndani ya Bunge hili la katiba,” alisema. 

Alisema walipoteza muda mwingi katika ibara ya kwanza ya sura ya kwanza kwa sababu zinashabihiana kwa kiasi kikubwa na ile ya sura ya sita “Na ndiyo maana tulipoteza muda mwingi sana katika ibara ya kwanza ya sura ya kwanza kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu inashabihiana kwa kiasi kibwa na sura ya sita…ukitoa neno shirikisho inamaana, inabidi ubadilishe kilichokuwamo katika Ibara ya kwanza ya sura ya pili,” alisema.

Aliwatoa wasiwasi Watanzania wote kuwa katika kamati hiyo hakuna miongozo wala taarifa nyingi kwa sababu wajumbe wote wanabishana kwa hoja zenye mashiko.Pia alisema wanakabiliwa na changamoto kuhusu upatikanaji wa theluthi mbili katika upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisema kamati hiyo imefanikiwa kupata theluthi mbili katika ibara ya sita na ya tisa ya sura ya kwanza. “Kanuni za Bunge hili bado hazituzuii…siyo kwamba haya maamuzi ni ya mwisho, bado tutaweza kwenda mbele ya Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kutoa taarifa yetu na kuendelea na hatua zinazofuata,”alisema.

Hata hivyo, alilalamikia kuwapo kwa muda mchache kwa ajili kujadili sura hizo mbili za Rasimu ya Katiba na kuwa walimwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kwa ajili ya kuongezewa muda.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa