Home » » LIPUMBA :SERKALI UMOJA WA KITAIFA Z'BAR HAIWEZEKANI KUVUNJWA

LIPUMBA :SERKALI UMOJA WA KITAIFA Z'BAR HAIWEZEKANI KUVUNJWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kuwaeleza maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho lililokutana Makao Makuu yao jijini Dar es Salaam juzi. Kulia ni Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, Abdul Kambaya.PICHA: SELEMANI MPOCHI
Wakati baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika moja ya mikutano yao ya hadhara iliyofanyika Zanzibar wiki iliyopita, wakipendekeza kuvunjwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema, haiwezi kuvunjika kwani ipo kikatiba na Wazanzibari ndiyo waliyoipendekeza.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. ibrahim Lipumba, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, hali ya uchumi na kisiasa nchini, maandalizi ya mkutano mkuu wa taifa na uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

“Baraza kuu linalaani kauli zilizotolewa katika mikutano ya CCM iliyofanyika Zanzibar zenye lengo la kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatokana na matakwa ya kura ya maoni ya Wazanzibari wote na imesaidia kuleta amani na utulivu Zanzibar,” alifafanua Prof. Lipumba na kuongeza:

“Kauli za kuchochea kuivunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, zinapandikiza mbegu ya chuki na vurugu inayoweza kusababisha maafa makubwa.”

Aliongeza kuwa  baraza hilo pia linalaani kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyoitoa katika mkutano huo wa CCM, kwamba mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, siyo raia wa Zanzibar, kwamba ni ya kibaguzi na inalenga kupandikiza chuki dhidi ya Wazanzibari na Watanzania wenye asili ya kihindi.

Kuhusu mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, Lipumba alisema, Baraza Kuu limepokea kwa masikitiko makubwa kuhusu mwenendo wake ambao kwa sasa upo katika hatua ya Bunge Maalumu la Katiba.

“Baraza Kuu linatambua kuwa kuna kila njama za kudharau maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hivyo linawataka wadau wote wa katiba ikiwamo serikali, vyama vya siasa na mamlaka zote kuiheshimu Rasimu ya Katiba, kuiboresha na kuhakikisha wananchi wanapata katiba waliyoipendekeza wao wenyewe,” alisema.

Alisema, baraza hilo pia limeshangazwa  na hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete, alipolihutubia Bunge la Katiba, Machi 21 mwaka huu kwamba ilidharau maoni ya wananchi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba na  ilitumia lugha ya kibaguzi na vitisho kuwa iwapo mfumo  wa   muungano wa serikali tatu ukipitishwa, jeshi litapindua nchi.

‘Baraza kuu la uongozi la taifa, linamtaka Rais Kikwete atambue kuwa yeye ndiye aliyeanzisha mchakato huu wa katiba kwa matakwa ya wananchi na kwamba mchakato huu ukikwama na nchi ikipata matatizo, yeye atakuwa mwajibikaji namba moja.”

Aliongeza kuwa baraza hilo linalaani hatua ya serikali ya kuifungia tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kuwanyima Watanzania fursa ya kupata nyaraka muhimu kuhusu Rasimu ya Katiba zilizoandaliwa na tume hiyo na aliitaka serikali kufungua tovuti hiyo kwani kwa kutofanya hivyo kutawanyima wananchi  haki ya kupata taarifa na kuibua wasiwasi wa kuchakachuliwa kwa baadhi ya nyaraka.

Alisema, wanaupongeza Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa) kwa maamuzi yake ya kujiondoa kwenye Bunge la Katiba, akisema bunge hilo limepoteza mwelekeo kwa wajumbe walio wengi kuacha kujadili rasimu iliyopelekwa na kushughulikia inayodaiwa kuwa na mfumo mpya ambao haukupendekezwa na wananchi.

Kadhalika alimpongeza Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kwa kukubali kulivunja baraza kivuli na kuvijumuisha vyama vingine vya siasa
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa