Home » » 'VIJANA JNGENI ARI YA KUJIAJIRI

'VIJANA JNGENI ARI YA KUJIAJIRI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein
 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amewataka vijana kujenga ari ya kujiajiri huku wakijizatiti kukabiliana na changamoto za ushindani katika soko la ajira.
Rais Shein alitoa wito huo jana alipokuwa akifungua kongamano la siku mbili kuhusu ajira kwa vijana linalofanyika katika ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

"Vijana mnapaswa kuukubali ukweli kuwa uwezo wa serikali wa kumpatia kila mhitimu ajira haupo, hivyo hamna budi kubadili mtazamo wenu wa ajira kwa kuwa tayari kujiajiri pamoja na kujiepusha na tabia ya kuchagua ajira bila sababu za msingi," alisema.

Alisema vijana hawana budi kuzingatia kaulimbiu ya kongamano hilo ambayo inawataka kubadilika na kuchangamkia kila fursa ya ajira stahiki.

Katika kuthibitisha kauli yake ufinyu wa nafasi za ajira serikalini, Rais Shein alieleza takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2010 ilipoingia Serikali ya Awamu ya Saba, imetoa nafasi za ajira 3,539 tu wakati kila mwaka maelfu ya wanafunzi wanahitimu elimu ya juu kutoka vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi. 

Dk. Shein aliwaeleza washirikiri wa kongamano hilo ambao wanatoka wilaya zote 10 za visiwa vya Unguja na Pemba serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira mazuri ambayo yatawezesha kutoa fursa zaidi za ajira kwa vijana zikiwa za kuajiriwa na kujiajiri.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ambapo wawekezaji zaidi waanzishe miradi na biashara ambazo zitatoa ajira kwa vijana pamoja na serikali kuanzisha mpango wa uwezeshaji kiuchumi wa wananchi wakiwemo vijana.

Katika risala ya vijana hao iliyosomwa na Lelya Mansoor Abdallah, mbali ya kuiomba serikali kuongeza fursa za elimu ya juu, pia waliomba kufanyiwa marekebisho ya mitaala ya vyuo ili kuwawezesha wahitimu kuajiriwa na kujiajiri.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Waziri wa Kazi na Utumishi wa Umma, Haji Omar Heri, aliwahakikishia vijana kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itayafanyia kazi matokeo ya kongamano hilo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

Alisema serikali imekichukua kwa uzito kilio cha Chama cha Waajiri Zanzibar (Zanema) cha kutaka serikali kuwandaa vijana wanaohitimu vyuoni wanaoweza kuajirika na kumudu majukumu yao ipasavyo.

Akitoa maelezo kuhusu washiriki wa kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Fatma Gharib Bilal, alisema kuwa miongoni mwa washiriki ni vijana walioajiriwa, waliojiajiri miongoni mwao wakiwamo waliopata mafanikio, walio nje ya ajira ambao wanatarajia kujiajiri, walio vyuoni pamoja na waajiri.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa