Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tumesikia matamshi ya mbunge wa Nkasi Kaskazini kupitia CCM,
Ally Mohammed Keissy alipochangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa akisema Zanzibar haichangii katika Muungano,
hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili.
Laiti kama angelijua kuwa matamshi yake yangeweza kuwatibua Wazanzibari, pengine asingesema hayo ambayo ameyasema.
Athari ya matamshi yake yanaakisi tatizo la msingi katika Muungano huu ambao umetimiza miaka 50.
Hatuwezi kumtupia lawama kwani ndiyo yaleyale
aliyoyasema mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba kwamba kuna dhana ya Tanzania Bara kuona kwamba Tanganyika ndiyo
Serikali ya Muungano au Tanganyika kuvaa koti la Muungano.
Nimkumbushe mbunge huyu kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilisita kuchangia suala la Muungano tangu mwaka 1984.
Sababu kuu iliyosababisha kufikia hatua hiyo ni
kwamba Zanzibar haifahamu ina wajibu wa kuchangia kiasi gani na mgawanyo
wa mapato ya Muungano ukoje?
Hadi leo Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania haifahamiki nini hasa inafanya, bado kuna giza nene
kuhusu mgawanyo wa masilahi na gharama za Serikali ya Muungano ikiwa ni
pamoja kugawana mapato, misaada ya kutoka nje masilahi mengine, ikiwamo
gesi asilia ambayo hadi naandika makala haya Zanzibar haipati kitu.
Kuna tetesi kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha imeshatoa mapendekezo ya namna
Zanzibar na Tanzania Bara zitakavyochangia gharama za uendeshaji wa
Serikali ya Muungano.
Taarifa zilizopo ni kuwa SMZ imeshatoa mapendelezo
yake muda mrefu wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inasemekana imo mbioni kufanyia kazi mapendelezo hayo.
Aidha, Serikali hizi mbili mwaka 1994 ziliomba
msaada wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuzishauri kuhusiana
na Benki Kuu (BoT), mgawanyo wa misaada na uhusiano wa kifedha.
Kwa msingi huo ndiyo sasa yanazuka hayo ya kusema
kuwa Zanzibar haijachangii gharama za uendeshaji wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano.
Pia, kuna suala la mapato yatokanayo na mafuta na
gesi asili. Licha ya suala hilo kuwa la Muungano, Zanzibar haijawahi
kupata gawio lake.
Wakati hayo yakiendelea, Zanzibar inahitaji
kuwahudumia watu wake katika afya, elimu, majisafi na salama, umeme na
mengineyo. Mambo hayo siyo ya Muungano.
Ukiacha hili la gesi asilia, kuna suala la hisa za Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, nalo ni kizungumkuti.
Ukiacha hili la gesi asilia, kuna suala la hisa za Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, nalo ni kizungumkuti.
Pia, kuna wizara na idara za serikali ambazo siyo
za Muungano, lakini zimewekwa katika Wizara za Muungano, nalo ni tatizo
jingine ambalo linatatiza suala zima la uchangiaji na ugawanaji wa
mapato.
Ndipo wengine wanapodai Serikali ya Tanganyika ‘imejibanza’ upenuni mwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mathalan, mambo ya kilimo, elimu ya msingi na
kati, tawala za mikoa na serikali za mitaa siyo katika mambo ya
Muungano, nani anayesimamia? Jibu ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Yapo mambo yanayolalamikiwa siku nyingi na
Zanzibar katika Muungano huu kama suala la uwakilishi wake kwenye Bodi
za Baraza la Mitihani (Necta), Shirika la Ndege (ATCL), Shirika la Simu
(TTCL). Inadaiwa kuwa Zanzibar haifaidiki kutokana na biashara ya
mashirika haya.
Malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa
kodi mara mbili wanapokwenda Tanzania Bara kwa bidhaa ambayo tayari
imeshalipiwa ushuru ambapo jambo hili limezungumzwa mara nyingi, lakini
hali ni ile ile.
Suala la uchumi siyo la Muungano kwa maana ya
kila upande una wizara yake inayoshughulikia uchumi, mipango na sera
zake za uchumi na bajeti yake.
Aidha, kila upande una mfuko wake mkuu wa
serikali na hivyo mapato yake, kila upande una jukumu la kushughulikia
huduma za jamii, miundombinu, kila upande una sera na sheria zake za
biashara na uwekezaji na hata sheria za ajira.
Wataalamu wa mambo ya katiba wanasema licha ya
ukweli huo, Katiba ya Muungano haiweki bayana na ndiyo inayofanya kusiwe
na majibu ya wazi ya suala hili kwa sababu kodi ya mapato, mikopo ya
nje na biashara za nje bado yamefanywa ni mambo ya Muungano.
Kodi ya mapato ambayo ni nyenzo kuu ya uchumi wa
visiwa ambao ni ‘service oriented’ badala ya kuwa ‘resource based’ kama
ilivyo kwa bara, bado ni jambo la Muungano kisera, ingawa mapato halisi
yanatumika Zanzibar .
Kingine katika muundo wa Muungano ni kwamba sera
za fedha na uhusiano wa kikanda upo chini ya Serikali ya Muungano bila
ya kuwa na uwazi wala sheria inayoilazimisha kushughulikia maslahi ya
kiuchumi ya Zanzibar.
Kwa misingi hiyo, ndiyo maana Dk Salmin Amour
‘Komandoo’ katika utawala wake wa awamu ya tano alitilia mkazo maeneo
huru kiuchumi , bandari huru na kampuni nyingine za kibiashara ikiwa
njia ya kujinasua na hali ngumu ya uchumi.
Ikiwa mfumo wa muundo wa Muungano utakuwa wa serikali tatu,
Zanzibar kwa jiografia yake inaweza kupata fedha nyingi za kigeni kwa
kutoa huduma za bandari na inaweza kuhudumia meli kubwa za tani
100,000.
Maumbile ya bahari ya Zanzibar yanaruhusu meli
kubwa kufunga gati wakati wote iwe maji yamekupwa au kujaa. Hii
itasaidia zile meli zinazozunguka Afrika Kusini na kufunga gati Dubai
sasa zinaweza kutumia bandari ya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha meli
kubwa za mizigo na hivyo kuchangia uchumi. Kukiwa na mfumo imara wa
shirikisho nina hakika Zanzibar baada ya miaka kumi ijayo inaweza
kufanya maajabu katika uchumi ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kiasi
cha kuwa ‘Singapore’ ya Afrika.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment