Home » » ATAKAYEKEJELI MAPINDUNZI Z'BAR KUKIONA CHA MOTO

ATAKAYEKEJELI MAPINDUNZI Z'BAR KUKIONA CHA MOTO

KAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seid Ali Idd, amesema Serikali itakuwa tayari kupambana na mtu au kundi lolote litakalothubutu kudhihaki au kukejeli Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, mwaka 1964.

Balozo Seif aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa ajili ya kuadhimisha miaka 51 tangu yafanyike Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yaliuangusha utawala wa kisultani.

Alisema umadhubuti wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ni ule ule wa mwaka 1964, hivyo ameonya kuwa Serikali haitamvumilia mtu atakayechezea Mapinduzi.

Alikumbusha kwamba Serikali hiyo ni ya wananchi wenyewe ambao hawako tayari kuona uhuru na ukombozi wao ukipuuzwa na kubezwa.

“Serikali yetu bado iko imara na wakati wote tuko macho dhidi ya chokochoko yoyote, tunashangaa baadhi ya watu sasa waliokataa kuyatambua Mapinduzi, eti nao wanaimba nyimbo za kusifu kwa unafiki,”alisema Balozi Seif.

Alisema unafiki wa watu hao hujidhihirisha kutokana na vitendo vyao kwa kuwa wanayoyasema ni mambo tofauti na yale yaliyoko kwenye mioyo yao na kuwataka wananchi wa Zanzibar kuwa macho na watu hao.

Akizungumzia umuhimu wa kulinda Muungano, Makamu wa Pili wa Rais alisema kitendo chochote cha kudhoofisha Muungano kamwe kisipewe nafasi, kwani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si wa makaratasi bali ni wa kindugu na damu.

“Kilichofanyika mwaka 1964 ilikuwa ni kurasimisha makubaliano ya udugu wetu, umoja wa watu wa Zanzibar na Tanganyika ni wa asili moja tokea zama na zama, hakuna mtu yeyote wa Zanzibar asiye na jamaa au ndugu Tanzania Bara,’alisema huku akishangiliwa.

Hata hivyo Balozi Seif aliwataka wanachamwa wa CCM wanaotokana na vyamna vya TANUA na ASP kuwa macho na maadui wa Muungano na Mapinduzi na kusema jukumu la kushinda katika uchaguzi mkuu wowote ni la jambo la kufa na kupona.

Alisema bila ya CCM kushinda na kuongoza dola Zanzibar na Tanzania Bara wananchi wanaweza kujikuta katika madhila na taharuki na kusema wapo baadhi ya wanasiasa wanapanga madhila ili kuwadhuru wengine.

Akizungumza katika ufunguzi wa matembezi hayo Mwenyekiti wa UVCCM Sadifa Khamiss Juma alisema wananchi wa Zanzibar kamwe hawatakubali kurudi katika zama za kutawaliwa na wakoloni mambo leo au wale wa kale.

Sadifa alisema Zanzibar ni nchi pekee iliyotawaliwa na wakoloni wawili kwa wakati mmoja na kwasababau hiyo tukio la Uhuru wa mwaka 1963 ni sawa na kitendo cha kuigiza kwasababu mkoloni mmoja aliondoka na kukabidhi madaraka kwa mwingine.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa