Juma Kaseja akifanya mazoezi
Hatimaye uongozi wa Yanga umetangaza rasmi kuachana na kipa
wake Juma Kaseja wakisema kuanzia sasa ni mchezaji huru. Awali kipa huyo
mkongwe aliamua kuipa kisogo timu hiyo akilalamikia kutolipwa sehemu ya
fedha zake za usajili pamoja na bima ya afya yake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro
alisema uongozi wao umefikia uamuzi huo baada ya Kaseja kuamua kuvunja
mkataba wake kwa kujiondoa katika kikosi hicho.
Muro alisema Kaseja aliamua kuwa nje ya uwanja kwa
muda wa wiki tatu mfululizo bila ya taarifa kwa waajiri wake kitendo
ambacho ni kinyume na sheria za kazi.
Alisema Yanga haidaiwi na Kaseja chochote na kipa
huyo aliyesajiliwa kwa miaka miwili Novemba 8, 2013 alilipwa kiasi cha
Sh20 milioni wakati akisajiliwa huku kiasi kingine akilipwa mapema mwaka
jana kabla ya kuanza kulalamika.
“Katika mkataba wetu na Kaseja hakuna kifungu
kinachosema tulitakiwa kumlipa lini hicho kiasi kilichosalia, lakini
Yanga tukamlipa fedha zake hata kabla ya kuanza kulalamika,” alisema
Muro.
“Ukiangalia barua yake pia Kaseja alilalamika
kwamba hapangwi katika timu, lakini kwa mujibu wa makocha waliokuwepo
wakati huo walituambia hakuwa na uwezo wa kucheza mechi labda tunampa
nafasi katika mechi dhidi ya CDA ya Dodoma na timu moja ya Shinyanga.
Aidha Muro alisema wakati Yanga ikifikia uamuzi
huo, uongozi wao unafikiria kufungua madai kwa kipa huyo kwa kutakiwa
kuilipa Yanga fidia ya siyo chini ya sh300 milioni kwa kitendo chake cha
kujiondoa katika timu yao.
Mwanzoni mwa mwezi huu katika taarifa iliyotolewa
na Kaseja kupitia kwa wakili wake, Samson Mbamba ilisema kuvunjika kwa
mkataba kati ya Yanga na mteja wetu Juma Kaseja kwa sababu kubwa moja ya
uongozi kukiuka kipengele kikubwa (fundamental term) kwa kutomlipa
katika muda mwafaka mteja wetu fedha za awamu ya pili ya usajili.
“Hata hivyo ilikuja kubainika kuwa kiasi cha fedha
kilichokuwa kikidaiwa kiliwekwa kwenye akaunti ya mteja wetu Oktoba 27,
2014, ikiwa ni takriban miezi tisa au kumi hivi baada ya muda
uliokubalika katika mkataba.
“Aidha fedha hiyo ililipwa kwenye akaunti bila
taarifa kwa mteja wetu kama ambavyo ingetakikana na baada ya kugundua
kuwa uongozi wa Yanga uliamua kuupa tena uhai (specific performance)
mkataba uliokwishavunjwa tangu Januari 15, 2014 na kuhalalisha upya
tena kwa kumlipa fedha za usajili iliyokuwa ikidaiwa.”
Hata hivyo, jana Mwanasheria Mbamba alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo mpaka pale atakapoonana na mteja wake.
“Siwezi kusema chochote mpaka nitakapokutana kwanza na Kaseja, si unajua tunafanya kazi kwa maelekezo.”
Mkurugenzi wa Mashindano TFF, Boniface Wambura alisema hawezi kulitolea ufafanuzi jambo hilo mpaka wapate taarifa kutoka Yanga.
“Tumesikia hizo habari, lakini hatuwezi kuzitolea
ufafanuzi kwa sasa mpaka tuone hizo sababu zao za kutolewa kwa uamuzi
huo ndipo tuzitolee tamko,” alisema Wambura.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment