Vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM kutoka Tanzania Bara na Visiwani
Zanzibar wakiandamana mjini Unguja juzi ikiwa ni sehemu ya shamra shamra
ya maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kilele cha
maadhimisho hayo ni leo.
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amewataka vijana kuendelea
kulinda misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa tukio hilo ni
mchakato uliotokana na madhila waliyofanyiwa wazawa wakati wa utawala wa
Sultani.
Dk Shein alitoa tamko hilo jana wakati akihutubia
wananchi kwenye Uwanja vya Maisara, wakati akipokea maandamano ya
kuwaenzi viongozi wa kitaifa baada ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ya lazima kutokana na wananchi kuchoshwa na manyanyaso ya wageni ndani ya ardhi yao.
“Baada ya Afro Shiraz kunyimwa ushindi katika kila
uchaguzi na uamuzi wa Uingereza kuipa Zanzibar ‘uhuru’ chini ya Sultan,
wazee wetu hawakuwa na namna zaidi ya kufanya mapinduzi kuirejesha nchi
mikononi mwa wazawa,” alisema Dk Shein.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Dk Shein aliwakumbusha
wananchi tukio la kuhuzunisha la utawala wa kikoloni kuwalazimisha
wazawa kuhudhuria sherehe za kumkabidhi Sultani nchi yao.
“Uhuru ule uliwasononesha wazee wetu na sisi tukiwa watoto, tulilazimishwa kuhudhuria,” alisema Dk Shein.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, Dk Shein
alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kufuata sheria na taratibu
wakati wa kufanya shughuli zao.
“Tofauti za kisiasa na vyama zisitufanye tukakiuka utaratibu wa kisheria,” alionya Dk Shein.
Alibainisha kuwa Zanzibar inaendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia kwa kufuata Katiba na sheria zilizopo.
Awali, Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis
alisema matembezi hayo ya vijana ni mchango wa kuimarisha na kuenzi
mapinduzi yaliyofanywa na vijana wenzao wa Afro Shirazi mwaka 1964,
ambao alisema walijitwisha jukumu kubwa la kuwakomboa wananchi wa
Zanzibar dhidi ya uonevu na udhalimu wa wakoloni wa kisultani.
“Umoja wa vijana wa Afro Shiraz tunaendelea
kuumbuka kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuleta mapinduzi. Tuna sababu ya
kuenzi kazi kubwa waliyofanya,” alisema mwenyekiti huyo.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Zanzibar Shaka Hamdu
Shaka alisema vijana 600 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara,
walishiriki matembezi hayo yaliyoanza Januari 6 mwaka huu katika Kijiji
cha Unguja Ukuu, Mkoa wa Kusini Unguja
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment