Home » » SHEIN: MUHIMU Z'BAR, MSUMBIJI, ZIBADILISHANE UTAALAM, UZOEFU.

SHEIN: MUHIMU Z'BAR, MSUMBIJI, ZIBADILISHANE UTAALAM, UZOEFU.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema wakati umefika kwa Zanzibar na Msumbiji kubadilishana uzoefu na utaalam katika sekta mbalimbali za maendeleo na uchumi ikiwa njia mojawapo ya kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya serikali na wananchi wa pande mbili hizo.
 
Akizungumza na Rais wa Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi Ikulu Zanzibar jana, Dk. Shein alimueleza Rais huyo kuwa historia inaonyesha kuwa uhusiano kati ya watu wa Zanzibar na Msumbuji umedumu kwa karne nyingi kabla ya uhuru hadi sasa ambapo watu wa pande mbili hizo wamekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu.
 
"Ni wakati mwafaka kwa pande hizo kuangalia namna zinavyoweza kutumia fursa zilizopo katika maeneo ya ushirikiano kuimarisha uhusiano kati yao na wananchi," alisema.
 
Dk. Shein alizitaja sekta za utalii na uvuvi kuwa ni maeneo ambayo nchi hizo zinaweza kubadilishana uzoefu.
 
Alimueleza Rais huyo kuwa eneo lingine la ushirikiano ni elimu na mafunzo kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Zusa) na vyuo vikuu vya Msumbiji.
 
Aliongeza kuwa sekta ya biashara ni sekta muhimu ambayo pande hizo zilikuwa zikishirikiana kwa miaka mingi na kudokeza kuwa kufuatia Serikali ya Zanzibar kununua meli mpya safari za kibiashara kati ya bandari za nchi hizo zinaweza kuanzishwa tena. Aidha,  Rais Shein alimpongeza Rais Nyusi kwa ushindi wake katika uchaguzi mkuu uliopita nchini Msumbiji kupitia chama cha Frelimo. 
 
Kwa upande wake, Nyusi wa Msumbiji alisema ziara yake nchini Tanzania ina lengo la kudhihirisha dhamira ya serikali na wananchi wa nchi yake kuimarisha uhusiano wake na serikali na wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Alieleza kuwa serikali na wananchi wa Msumbiji wanathamini mno uhusiano wao na serikali na wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Rais Nyusi alisema wananchi wengi wa Msumbiji wamekuwa wakiishi nchini Tanzania kwa furaha na mapenzi makubwa kutoka kwa ndugu zao wa Tanzania, hivyo ni jambo la kujivunia kwao.
 
Pia alisema Msumbiji na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri wa kisiasa na kidiplomasia hivyo ni wakati sasa kupanua uhusiano huo katika maeneo mengine yakiwamo ya uchumi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa