Home » » UPOTOSHAJI WA TAKWIMU WAKWAMISHA MAENDELEO

UPOTOSHAJI WA TAKWIMU WAKWAMISHA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


UKOSEFU wa takwimu sahihi katika masuala mbalimbali umeelezwa kuchangia kutopiga hatua kwenye mipango ya kimaendeleo inayopangwa na serikali juu ya wananchi.

Aidha upotoshaji wa takwimu hizo unaofanywa na baadhi ya watendaji kwa kutaka kujinufaisha wenyewe pia umekuwa ukichangia kuchelewa hatua za kimaendeleo.
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Zanzibar, Amina Shaaban wakati akifungua semina ya siku moja ya kujadili malengo ya milenia baada ya mwaka 2015 iliyofanyika mjini hapa.
Amina alisema kuwa takwimu ndiyo zinaonesha hali halisi na pia zinawezesha fedha kutoka kulingana na mahitaji, hivyo ni muhimu kuzingatiwa kwa jambo hilo ili mipango ya maendelo iweze kufanyika kwa wakati.
“Kulikuwa na kamati ile ya ufundi na ya muda, siku hizi hazipo kama zimekufa ni vyema zikarudishwa tena maana zilikuwa na jukumu la ufuatiliaji na kutukumbusha mara kwa mara,” alisema Amina.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi (ESRF), Dk Tausi Kida, Dk Oswald Mashindano alisema, semina hiyo inalenga kujadili na kupata taarifa ya sehemu ya utekelezaji wa malengo ya milenia kabla ya kumalizika Septemba, mwaka huu.
Aidha alisema, nchi nyingi hazijakuwa na uwezo wa kutekeleza malengo ya milenia ikiwemo Tanzania, hivyo kutokana na hali hiyo ilikubalika kuwepo kwa ajenda mpya ya maendeleo baada ya Septemba, mwaka huu.
“Kwa sisi Tanzania kidogo tuna bahati ya kupiga hatua kidogo, lakini pamoja na kutimiza baadhi ya malengo, bado kuna maeneo ambayo hatujafanikiwa sana na moja kati ya sababu iliyofanya tukwame ni pamoja na ukuaji wetu wa uchumi,” alisema.
Semina hiyo iliwashirikisha wataalamu wa Tume ya Mipango ya Zanzibar na taasisi nyingine za serikali ilikuwa inalenga kuwajengea uwezo na kujadili ajenda 17 za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na mipango ya maendeleo baada ya kukamilika kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Septemba, mwaka huu.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa