Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),
imesema Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kupita kiasi pamoja na kufanya
vitendo vya udhalilishaji wakati wa kumkamata Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi 32 wa chama hicho.
Prof. Lipumba na wafuasi hao walikamatwa na Jeshi la Polisi Januari
27, mwaka huu wakati wa vurugu za kuzuia wanachama wa CUF waliotaka
kufanya maandamano kuelekea eneo la Zakhem, Mbagala, jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kufanya kumbukumbu ya miaka 14 ya mauaji ya wenzao
waliouawa Januari 27, 2001 na Jeshi la Polisi Zanzibar.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga, alikuwa akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kutoa taarifa ya uchunguzi
wa tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi za kuwapiga na kuwadhalilisha
viongozi na wafuasi wa CUF ambao ulianza Februari 3 na kukamilika Mei
15, mwaka huu.
Nyanduga alisema uchunguzi wa tukio hilo uliofanywa na tume hiyo
ulibaini kuwa Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kupita kiasi na kutumia
mabomu ya machozi hata pale ambapo haikuhitajika kufanya hivyo na
kusababisha majeraha kwa viongozi na wafuasi wa CUF.
Alisema jeshi hilo pia lilikiuka misingi ya utawala bora kutokana
na maofisa na askari kushindwa kuheshimu haki za binadamu na
kutozingatia matakwa ya sheria zinazoongoza jeshi hilo, kufanya
udhalilishaji kwa wanachama wawili wa CUF ambao ni wanawake wakati wa
kuwakamata na kuwapeleka mahabusu ya gereza la Segerea.
MAPENDEKEZO
Nyanduga alisema kutokana na hali hiyo, tume imetoa mapendekezo
ambayo ni kulitaka Jeshi la Polisi liwe kuzingatia kanuni, sheria, haki
za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu
yake ya kila siku na pia kutolewe mafunzo kwa maofisa na askari
wanaoratibu na kushughulikia masuala ya maandamano, mikutano ya raia na
shughuli za vyama vya siasa.
Alisema mapendekezo mengine ni kuwa maofisa na askari wa jeshi hilo
wapatiwe mafunzo ya mara kwa mara yahusuyo haki za binadamu na misingi
ya utawala bora na wazingatie uhuru wa vyombo vya habari.
Nyanduga alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza imependekeza
lizuiwe mara moja kufanya upekuzi wa watuhumiwa na kuepuka udhalilishaji
kwa heshima na utu wa binadamu kwani ni kinyume cha kifungu cha 12(2)
na 13(6) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kwa upande wa CUF, kimetakiwa kitafute namna ya kuboresha
mahusiano na Jeshi la Polisi ili kuondoa mivutano isiyo na tija katika
shughuli za kisiasa na kizingatie sheria za nchi na ibara ya 147 (1) ya
Katiba inayozuia chama chochote cha siasa kuwa na kikundi chenye mtazamo
wa kijeshi.
KAULI YA CHIKAWE
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, akizungumza na
NIPASHE kuhusu mapendekezo ya tume, alisema kimsingi, Jeshi la Polisi
limepewa jukumu la kulinda usalama wa nchi na raia wake na kwamba
litazingatia haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Sisi hatutaki baadaye tuje tuanze kulaumiwa mambo yakiwa mabaya,
ndiyo maana tunasema usalama kwanza mambo mengine baadaye,” alisema
Chikawe.
Jeshi la Polisi Januari 27, mwaka huu lilitumia nguvu kuwatawanya
wafuasi wa CUF kwa kurusha mabomu, risasi za moto na maji ya kuwasha na
kumkamata Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi
wengine 32.
Nguvu hiyo ya polisi ilitumika wakati wa kuzuia msafara wa
mwenyekiti huyo wa CUF kuelekea eneo la Zakhem, Mbagala kulikokuwa
kumeandaliwa mkutano wa hadhara uliokuwa na lengo la kutoa taarifa kwa
wafuasi waliokuwa wamekusanyika kwa kuwa mkutano na maandamano
yamezuiliwa na polisi.
Mkutano huo ambao ulikuwa utanguliwe na maadamano kutoka ofisi za
wilaya ya Temeke kwenda Zakhem kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 14 ya
mauaji ya wafuasi wake zaidi ya 30 waliouawa Januari 27, 2001 na Jeshi
la Polisi Zanzibar wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi
wa Rais wa Zanzibar wa mwaka 2000.
Kutokana na purukushani hizo ilidaiwa kuwa polisi wenye silaha na
virungu walitembeza kichapo kikali kwa wafuasi waliokaidi amri ya polisi
kuwataka watawanyike, huku wakiwashusha waliokuwa kwenye magari.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment