Home » » Shaka: Dk. Shein atashinda urais kwa hoja, mafanikio.

Shaka: Dk. Shein atashinda urais kwa hoja, mafanikio.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein (pichani), atashinda kwa kishindo na kumtupa mbali mgombea mwenzake wa nafasi hiyo kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, kutokana kuwa na sera nzuri na kutumia ushawishi wa nguvu ya hoja na  mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana katika utawala wake pamoja na kuongoza vizuri na kwa hekima Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo.
 
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, wakati akizungumza na kituo kimoja cha televisheni mjini hapa  jana.
 
Katibu Mkuu huyo wa UVCCM yupo mkoani hapa kwa ziara ya siku mbili akifanya mikutano ya kampeni za CCM pamoja na kuwanadi mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, mgombea ubunge wa Morogoro Mjini kupitia chama hicho, Mohamed Aboud na wagombea udiwani.
 
Alisema Dk. Shein amejiegemeza katika siasa za kati na  za wastani, zinazozingatia  mapatano, mshikamano na maridhiano na kukwepa siasa za shari, huku akibebwa na rekodi ya kupaisha uchumi wa Zanzibar kutoka asilimia 4.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia  7.2, mwaka huu.
 
“Dk. Shein aliiingia madarakani mwaka 2010 na kuikuta Zanzibar ikiwa imekatika katika mapande ya uhasama, chuki na mgawanyiko wa kijamii, akafanikiwa kuifanya yenye umoja mpya na yenye maridhiano hadi sasa. alisema”
“Zanzibar ilikumbwa na misukosuko, mivutano ya kisiasa na kupwaya kwa  mahusiano kufuatia matokeo ya chaguzi kuu za mwaka 1995, 2000 na 2005 ambazo zililalamikiwa na upinzani bila sababu za msingi, huku baadhi ya taasisi za kimataifa zikizuia misaada lakini sasa visiwa hivyo viko salama chini ya mikono ya Dk. Shein,’ alisema.
 
Alisema tangu kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 baada ya kufanyika mazungumzo ya upatanishi na maridhiano visiwani humo, Dk. Shein amekuwa akiendesha kampeni za kistaarabu hadi za mwaka huu.
 
“Amebaki katika msimamo wake ule ule, kila mtu anashuhudia akifanya kampeni za nguvu ya hoja, sera na matokeo yatapotangazwa baadae mwezi huu ataibuka mshindi dhidi ya mgombea urais wa Cuf,” alisema Shaka.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa