Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkurugenzi
Mtendaji Kamisheni ya Maafa Zanzibar ndugu Ali Juma Hamad akifungua
mafunzo ya waandishi wa habari juu ya kujikinga na ugonjwa wa
kipindupindu katika Ukumbi wa gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini
Zanzibar, (kulia) daktari dhamana Kanda ya Unguja Dkt Fadhili Mohd na
(kushoto) Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirmay. Picha na Makame
Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Washiriki
wa mafunzo hayo wakimsikiliza kwa makini Daktari dhamana Kanda ya
Unguja Dkt. Fadhili Mohamed alipokuwa akielezea njia za kukabiliana na
kipindupindu katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika Ukumbi wa
Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini Zanzibar. Picha na Makame
Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Rafii Haji Mkame akiwasilisha mada
ya wajibu wa waandishi wa habari katika kukabiliana na maradhi ya
miripuko katika mafunzo yaliyofanyika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya
Mombasa Mjini Zanzibar.
Katibu
wa Jumuiya ya Maafisa wa Afya Zanzibar Ahmed Suleiman Said akitoa elimu
ya kupambana na maradhi ya kipindupindu kwa wananchi wa shehia ya
Shaurimoyo Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Baadhi ya
wananchi wa shehia ya Shaurimoyo Mjini Zanzibar wakifuatilia juu ya
elimu ya ugonjwa wa Kipindupindu iliyotolewa na Jumuiya ya Maafisa wa
Afya Zanzibar.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mwashungi Tahir – Maelezo Zanzibar.
Daktari dhamana kanda ya Unguja Dkt. Fadhil Mohammed Abdallah
amewataka wananchi kuchukua tahadhari kuhusu maradhi ya kipindupindu
ambayo kwa sasa ni tishio kubwa Zanzibar.
Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa
kwenye mafunzo ya waandishi wa habari juu ya kujikinga na ugonjwa huo
ambao bado unaendelea katika sehemu mbali mbali Zanzibar.
Amesisitiza kuchukuliwa tahadhari zaidi kupambana na maradhi ya
kipindu pindu ikiwemo kuweka mazingira safi, kufuata masharti ya
afya, kuchemsha maji ya kunywa ama kutumia maji yaliyotiwa dawa ya
kuulia bektiria wanaosababisha maradhi hayo..
Dkt. Fadhil amewataka wananchi kuacha tabia ya kula ovyo
njiani, kukosha matunda na mboga mboga kabla ya kula na kuchukua
tahadhari kubwa wakati wa kumshughulikia maiti ya maradhi ya kipindu
pindu kwani ni miongoni mwa njia za maambukizi ya maradhi hayo.
Amewataka waandishi wa habari kutekeleza majuku yao ya kutoa
elimu kwa wananchi ili wapate uelewa mkubwa zaidi kukabiliana na
maradhi hayo.
Amesema maradhi ya kipindu pindu ingawa ni tishio kwa maisha ya
wananchi lakini ni rahisi zaidi kuyadhibiti kuliko maradhi mengine iwapo
wananchi watafuata masharti ya afya.
“Waandishi wa habari mnao mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa
jamii katika kukabiliana na maradhi ya kipindupindu hivyo tunategemea
mashirikiano makubwa kutoka kwenu,” alisisitiza Dkt. Fadhili
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Maafa
Zanzibar ndugu Ali Juma Hamad amesema juhudi za pamoja zinahitajika
katika kukabiliana na kipindupindu na mchango wa kila mtu na taasisi
unahitajika.
Amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na maradhi
hayo tokea yalipogundulika mwezi Septemba mwaka jana ikiwa ni kipindi
cha jua kali, kuchukua muda mrefu na kusambaa sehemu mbali mbali za
Unguja na Pemba kinyume na watu walivyozoea vipindi vya nyuma.
Akiwasilisha mada ya majukumu ya vyombo vya Habari katika
kudhibiti miripuko ya maradhi ya kuambukiza, Mkurugenzi wa Idara y
Habari Maelezo Zanzibar Rafii Haji Makame amesema vyombo hiyo
vinajukumu la lazima katika kusaidia umma kudhibiti vifo na athari
nyengine za kiuchumi na kijamii zinazosababishwa na miripuko ya maradhi .
Katika kufanikisha majukumu hayo Mkurugenzi Rafii ametaka
kuongezwa ushirikiano kati ya vyombo vya habari na sekta ya afya ili
kupata taarifa sahihi kwa wakati katika kufikisha ujumbe kwa umma.
Aidha amesema utoaji wa elimu ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza
kupitia vyombo vya habari liwe suala endelevu ili jamii iweze kupata
uwelewa na kubadilika kitabia.
Jumla ya kambi 18 zilifunguliwa na kuhudumia wagonjwa 1066 Unguja
na Pemba na kati yao wagonjwa 22 walifariki. Hivi sasa kuna kambi nne
tu zinazoendelea kupokea wagonjwa katika kisiwa cha Unguja.
Wakati huo huo Katibu wa Jumuiya ya maafisa wa afya Zanzibar
Ahmed Suleiman Saidi amewashauri wananchi wa shehia ya Shaurimoyo
kubadili tabia na kuweka mazingira wanayoishi katika hali ya usafi ili
kujikinga na kipindupindu.
Alitoa ushauri huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa shehia
hiyo katika skuli ya Shaurimoyo walipowatembelea kutoa taaluma juu
yamaradhi hayo kwa vile shehia hiyo ni miongozi kati ya shehia
zilizoathirika na kipindupindu.
0 comments:
Post a Comment