Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaagiza viongozi wake kuzisoma
vizuri Katiba ya CCM, Kanuni za maadili na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka
1984, ili wawe na uwezo wa kujibu hoja za baadhi ya watu wanaosambaza
fitna na uzushi wa kukichafua chama hicho.
Kimesema
kiongozi yeyote mwenye uwezo na uelewa mzuri juu ya miongozo hiyo
hawezi kuyumbishwa na kauli na maneno ya mitaani badala yake atakuwa na
msimamo imara wa kusimamia maslahi ya chama kupitia vikao halali.
Agizo
hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
wakati akizungumza na viongozi mbali mbali wa Chama kuanzia ngazi za
matawi hadi wilaya huko katika Wilaya ya Amani Kichama, Unguja.
Aliwasihi
viongozi hao kutumia vikao halali vinavyokubalika kikanuni kujadili
changamoto na kasoro zinazojitokeza ndani ya chama kwa lengo la kuepuka
maneno ya mitaani yanayoweza kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima
ndani ya CCM.
Alisema
baada ya chama hicho kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio
uliofanyika Machi 20 mwaka huu kwa asilimia 91, kilichobaki kwa sasa ni
viongozi na wanachama kushirikiana vizuri na Rais, Wabunge, Wawakilishi
na Madiwani kusimamia vizuri Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho yam waka
2015/2020.
“
Sisi viongozi tukiendelea kuwa wamoja na wenye kushirikiana kwa lengo
la kusimamia maslahi ya CCM kwa vitendo basi, naamini kwamba chama chetu
nacho kitaendelea kuwa imara na kushinda kwa kila uchaguzi.
Pia
tujue kwamba ushindi wa uchaguzi mkuu wa marudio ndio mwanzo wa
kujipanga kimikakati kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, kwani hakuna muda
tena wa kusubiri ni lazima tuwe karibu zaidi na wanachama wetu ambao
ndiyo wapiga kura wetu.”, alisisitiza Vuai huku akiwasihi vuiongozi hao
kusoma alama za nyakati kwa kutathimini changamoto na kasoro zilizotokea
katika uchaguzi mkuu uliopita ili zisizokee tena katika uchaguzi ujao.
Naibu
Katibu Mkuu huyo, aliendelea kufafanua kwamba CCM ni chama chenye asili
ya amani na utulivu na kinachoamini kwamba umoja na msikamano ndiyo
fursa ya kuifikisha katika kilele cha Zanzibar na maendeleo endelevu ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia
suala la ajira, Vuai aliwashauri vijana kutokata tamaa kwani CCM
inaendelea kuikumbusha serikali kutafuta njia mbadala za kuhakikisha
vijana wenye sifa, vipaji,uwezo na maarifa ya ujuzi mbali mbali wa chama
hicho wananufaika na matunda ya ajira kutoka serikalini ama sekta
binafsi.
Aidha
Naibu Katibu Mkuu huyo, alilaani vikali kitendo cha Naibu Katibu Mkuu
wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika ziara yake ya Pemba cha
kuwakataza wananchi hasa wafuasi wake wasilipe kodi na kuwapandikiza
mbegu za chuki zinazolenga kuingiza nchi katika migogoro inayoweza
kuathiri uchumi wa nchi.
Alisema
kitendo hicho hakikubaliki kwani kinavunja sheria za nchi na Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984, kwa makusudi jambo linalotakiwa kuchukuliwa
hatua za kisheria na vyombo vya dola kabla nchi haijangia katika
machafuko.
“Sio
kwamba serikali inamuogopa Maalim Seif bali inafanya kila jambo kwa
kufuata sheria na Katiba ya nchi, lakini pia ni lazima tukumbuke kwamba
hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria.”, alisema Vuai na kuwasihi wananchi
hasa wafuasi wa CCM wasiwe na jazba na watulie huku wakisubiri mamlaka
husika zichukue hatua kwa watu wanaovunja sheria za nchi.
Naye
Katibu wa CCM Wilaya ya Amani Kichama, Abdallah Mwinyi alimuahidi Naibu
Katibu Mkuu huyo kuyafanyia kazi mambo yote yaliyotolewa kama nasaha na
ushauri kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya chama
hicho.
Nao
baadhi ya viongozi wa ngazi mbali mbali waliohudhuria kikao hicho,
wameelezea kuridhishwa kwao na mikakati mizuri iliyopo ndani ya chama
itakayosaidia kufanikisha ushindi wa dola katika uchaguzi mkuu 2020.
Pamoja
na hayo wameahidi kuendelea kuwa wamoja katika kulinda maslahi ya CCM
kwani ndiyo chama pekee kinachojali na kuthamini utu wa wananchi kupitia
kauli njema za kuhimiza amani na utulivu wa nchi.
0 comments:
Post a Comment