Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
SERIKALI
ya Mapinduzi Zanzibar imewataka Wazazi, Walezi na Wazee kuwalinda
watoto wao dhidi ya Mazingira hatari yanayowazunguka ili kuwaepusha na
athari za vifo pamoja na ulemavu.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar, Mauldine Castiko
wakati akiwafariji wahanga wa tukio la vifo vya watoto wawili
waliotumbukia katika Kisima cha Maji na kupoteza maisha huko katika
mitaa ya Tomondo Uzi, Unguja.
Alisema
wazazi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuwa waangalifu katika mazingira
wanayoishi kwa kuyaweka katika hali ya usalama ili kuwaepusha na madhara
watoto wadogo yanayoweza kuwasababishia vifo na hatari zingine
zinazoepukika.
Castiko
alitoa mkono wa pole kwa familia hiyo na kuwaomba waendelee kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa watoto hao wasiokuwa
na hatia.
Aliisihi
familia hiyo kuendelea kuvumilia katika kipindi kigumu cha msiba huku
watu waliohusika na uzembe wa kusababisha vifo vya watoto hao wachukue
juhudi za haraka kwa kufunika Kisima hicho ili kisiendelee kuhatarisha
maisha ya watoto wengine mtaani.
Alisema
serikali imesikitishwa na tukio hilo la vifo vya watoto wasiokuwa na
hatia na kuahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa familia hiyo.
Alizitaka
mamlaka zinazohusika na masuala ya ulinzi wa Raia na Mali zao
kuendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ili watu
watakaobainika kuhusika kwa uzembe na tukio wachukuliwe hatua za
kisheria.
“Familia, Ndugu na Jamaa wa marehemu nakupeni pole na kukuombeni muendelee kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Lakini
pia nachukua fursa hii kuwaomba wazazi na walezi kuwa makini na watoto
wenu hasa awa wadogo kwani mazingira wanayokuwa wakicheza mengi hayana
usalama juu ya maisha yao.”, alisisitiza Waziri huyo na kuongeza kuwa
serikali haitowavumilia watu wanaohatarisha maisha ya watoto kwa
makusudi na hatakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua za
kisheria.
Waziri
huyo alifafanua kwamba Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 pamoja na
Mikataba mbali mbali ya Kimataifa inayohusika na Haki za Binadamu
iliyoridhiwa na serikali ya Tanzania inatambua na kutetea haki za Watoto
kuhakikisha wanapata ulinzi wa kuishi na huduma mbali mbali za msingi
kama walivyo watu wengine.
Alisema
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira rafiki ya
kuhakikisha maisha ya watoto yanakuwa salama wakati wote wakiwa ndani
na nje ya familia zao huku ikiimarisha sheria na miongozo ya kusimamia
haki zao Kikatiba.
Alitoa
agizo kwa wananchi wote wa Zanzibar wanaomiliki visima vya maji ama
kuchimba mashimo mbali mbali yanayoweza kuhatarisha maisha ya watoto,
kufukia ama kuvifunika visihatarishe maisha ya watoto wengine.
Aidha
alisema jamii inatakiwa kuwa makini na watoto wadogo hasa kwa kipindi
hiki cha maradhi ya miripuko ya Kipindupindu kwa kuwaepusha watoto
wasile wala kunywa maji machafu na vyakula visivyokuwa salama kwa afya
zao.
“
Kuna baadhi ya familia hawafutilii mwenendo wa watoto wao pindi
wanapokuwa nje ya majumba yao kujua wanakula nini wala wanacheza katika
mazingira gani hali ambayo inaweza kuwaweka katika mazingira hatarishi
watoto wetu.”, alisema Waziri huyo.
Naye
Mama mzazi wa watoto hao, Mariam Hassan alishukuru ujio wa kiongozi
huyo na kueleza kwamba vifo vya watoto hao ni pigo kubwa kwa familia
yake.
Alisema
kwamba watoto hao walikuwa mazingira ya mtaani wakicheza ambapo yeye
alikuwa akiendelea na harakati za kuandaa chakula cha mchana ghafla
majira ya saa 7:30 mchana akaambiwa kwamba watoto wake wamedondoka
katika kisima cha jirani yao hapo mtaani.
Baada
ya kupata taarifa hiyo alifika katika kisima hicho ambapo alikuwa watu
mbali mbali wakiendelea na juhudi za kuokoa maisha ya watoto hao lakini
walipotolewa walikutwa washafariki kwani haikujulikana wameingia wakati
gani.
Aliwataja
watoto hao kuwa ni Yussuf Faki Juma mwenye umri wa miaka miwili(2) na
Muhamadi Ali Abdallah umri wa mwaka 1 na miezi nane wote wakiwa watoto
wa familia moja.
0 comments:
Post a Comment