WAZIRI wa Fedha Mipango na Uchumi, Dk Khalid Salum Mohamed leo
atawasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016-2017, iliyoweka
kipaumbele katika kuimarisha sekta ya elimu na miundombinu kwa kutumia
fedha za makusanyo ya kodi.
Akitoa muhtasari na muelekeo wa bajeti hiyo Dk Salum alisema Serikali
inakadiria kutumia Sh bilioni 841.5 kwa kazi za kawaida na Sh bilioni
395.9 kwa shughuli za maendeleo. Aidha alisema mkazo umewekwa katika
makusanyo ya kodi huku taasisi zenye majukumu hayo zikitarajiwa
kukusanya Sh bilioni 482.4 kutoka katika vyanzo vya ndani.
Alisema Bodi ya Mapato ya Zanzibar itakusanya Sh bilioni 237.4 na
Mamlaka ya Mapato (TRA) itakusanya Sh bilioni 188.8. “Bajeti ya mwaka
huu serikali haitopandisha kodi ya aina yoyote na badala yake itajikita
katika kuimarisha usimamizi na utendaji wa ndani katika makusanyo ya
kodi,” alisema Dk Salum.
Alisema mikakati ya serikali ni kubana matumizi na kuwa makini katika
kutumia fedha za bajeti kwa mujibu wa uwezo wa Serikali katika kufanya
makusanyo ya fedha, ambapo mkazo umewekwa katika kulipa madeni ya walimu
na viinua mgongo.
Dk Salum alisema kwa mara ya kwanza Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, inatarajia kufaidika na fedha za kodi ya mapato inayotokana na
watumishi wa Serikali ya Muungano waliopo Zanzibar, inayotarajiwa
kufikia Sh bilioni 21.0.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment