WAZIRI wa Habari Utangazaji, Utalii na Michezo wa Zanzibar, Rashid
Ali Juma amesema mabadiliko makubwa yanakuja katika taasisi na vyombo
vya habari vilivyopo chini ya Serikali hiyo.
Kwamba lengo ni kuleta ufanisi na uwajibikaji katika sehemu za kazi, ikiwamo kuundwa kwa bodi mpya.
Juma alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwa vyombo
vya habari, vinavyomilikiwa na Serikali ya Zanzibar ikiwamo gazeti la
Zanzibar- Leo, ambapo wafanyakazi na waandishi wa habari walielezea
kutoridhishwa na mazingira ya kazi yaliyopo hapo na suala la uadilifu
katika masuala ya fedha.
Alitaja hatua zitakazochukuliwa kuwa ni pamoja na kuundwa kwa Bodi
katika taasisi hizo zenye uwezo na kuleta mabadiliko makubwa, ikiwamo
kufanya biashara yenye faida.
“Tunakusudia kufanya marekebisho makubwa katika taasisi za habari na
nyingine ziliopo chini ya Wizara ya Habari kwa lengo la kuleta ufanisi
wa kazi na kuondosha malalamiko,” alisema waziri huyo.
Waziri Juma akiwa katika gazeti la ZanzibarLeo, aliwataka kuunda timu
imara itakayofanya kazi ya kukusanya madeni yanayodai gazeti hilo
kutoka kwa taasisi mbalimbali za serikali, yanayofikia Sh milioni 300.
Aliwataka watendaji katika masuala ya fedha, kufuatilia madeni yote
kujua nani amelipa na nani anadaiwa, ikiwa ni moja ya hatua ya kulifanya
shirika hilo kujiendesha bila kutegemea ruzuku serikalini.
“Kazi ya kufuatilia na kutafuta madeni yanayotokana na mauzo ya
magazeti pamoja na matangazo yapo kwa idara ya fedha ambao wao ndiyo
watakaofahamu nani amelipa fedha na nani hajalipa na njia za kupata
fedha hizo,” alisema Juma.
Baadhi ya waandishi wa habari waliozungumza, kwa nyakati tofauti
walisema kwamba utendaji chini ya kiwango katika idara ya uhasibu, ndiyo
chanzo cha kulifanya Shirika la Magazeti la Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kuyumba na kushindwa kujiendesha kwa faida.
Mwandishi wa habari mwandamizi, Mwantanga Ame, alisema ipo haja ya
kuwapo wafanyakazi watakaofuatilia na kujua hatma ya madeni ya shirika
yanayotokana na matangazo yanayotangazwa na taasisi na wizara pamoja na
mashirika ya umma.
“Tunakabiliwa na tatizo kubwa la mzigo wa madeni tunayodai kutoka
Serikali na taasisi binafsi ambapo udhaifu upo katika suala zima la
ufuatiliaji na utoaji wa risiti,” alisema.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment