WATUMISHI wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na idara
na taasisi zake wameipongeza hotuba ya Rais Ali Mohamed Shein katika
kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani ya kutangaza kutekeleza ahadi ya
kuongeza kima cha chini cha mishahara kufikia Sh 300,000 kuwa itaongeza
ufanisi wa kazi na ari ya uzalishaji mali.
Baadhi ya wafanyakazi waliohojiwa walisema Dk Shein ameonesha uwezo
wa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo ambazo alizitoa kwa nyakati
tofauti, ikiwemo kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu, kwa kusema
akichaguliwa kuongoza awamu ya pili ataongeza mishahara katika kipindi
cha mwaka wa kwanza wa fedha.
Ali Issa ambaye ni mfanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
alisema wamefurahishwa na uamuzi huo ambao sasa utaongeza ari ya kufanya
kazi na kupambana na hali ngumu ya maisha.
“Nimefurahishwa na uamuzi uliochukuliwa na Rais Shein wa kuongeza
kima cha chini cha mshahara kufikia Sh 300,000 utasaidia kuongeza ari ya
kazi na kuleta ufanisi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wafanyakazi na
kupambana na ugumu wa maisha,” alisema Issa.
Tukena Abdalla Amour anayefanya kazi Wizara ya Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi alisema Rais Shein ameonesha muungwana anavyotakiwa kuwa
kwamba akiahidi kwa kutoa ahadi huitekeleza bila ya ajizi kwa wakati
mwafaka.
Alisema ahadi aliyoitoa katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu
baadhi ya wananchi waliikejeli, ikiwemo wapinzani wa vyama vya siasa na
kusema haitekelezeki kwa sababu nchi haina uchumi imara ambayo ilikuwa
na lengo la kutaka kuwavunja moyo watumishi wa serikali tu.
“Mimi nimefurahishwa na kauli ya Rais Shein ya kutangaza kima cha
chini cha mshahara kupanda kutoka Sh 150,000 hadi 300,000 ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi yake aliyokuwa akituambia katika kipindi cha
mikutano ya hadhara ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwamba
nikichaguliwa nitaongeza mishahara,” alisema.
Hassan Iddi wa sekta ya binafsi ya hoteli za kitalii aliwataka
wawekezaji binafsi nao kuitikia mwito wa rais kuongeza mishahara ili
iende sambamba na hali ya maisha iliyopo kwani utalii ndiyo tegemeo la
uchumi wa Zanzibar kwa sasa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (ZATUC),
Khamis Mwinyi alisema hotuba ya rais ni dira kwa wafanyakazi na
watumishi wa serikali ambao ndiyo wanaotegemewa kutekeleza majukumu
mbalimbali.
Alisema wamefurahishwa na rais ambaye amedhihirisha kwamba ni mtu
anayewapenda wafanyakazi kwa kuzingatia maslahi bora kwa mujibu wa hali
ya maisha ilivyo kwani ukweli ni kwamba maisha yamepanda.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment