TAARIFA YA CCM ZANZIBAR KWA VYOMBO VYA HABARI
ILIYOTOLEWA NA AFISI KUU YA CCM ZANZIBAR KUHUSIANA NA PROPAGANDA CHAFU
ZINAZOTOLEWA NA KATIBU MKUU WA CUF MAALIM SEIF SHARIF HAMAD DHIDI YA SERIKALI
YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR NA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kinatoa indhari kwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuhusiana na Propaganda chafu, za uongo na upotoshaji zinazoendelea kusambazwa
na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ndani na nje ya nchi dhidi ya
Serikali mbili zilizoko madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi na viongozi
wake.
CCM Zanzibar tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa marejeo
imekuwa ikishuhudia matukio mbali mbali ya hujuma ambazo chanzo chake ni kauli
za uchochezi, uongo na upotoshaji zilizotolewa hadharani na Katibu Mkuu wa CUF
Maalim Seif Sharif Hamad katika ziara zake kwenye maeneo tofauti Unguja, Pemba
na nje ya Zanzibar.
Wana-CCM, viongozi na wananchi wa Zanzibar wameshuhudia kuchomwa
kwa mashamba ya mikarafuu, kuharibiwa mazao ya wakulima, watu hasa wanachama na
wafuasi wa CCM kuchomewa nyumba zao, kuitishwa migomo, wananchi kushawishiwa
kutoitambua serikali halali iliyoko madarakani pamoja na matukio kadhaa yenye
kuashiria uvunjifu wa amani na uhujumu wa uchumi wa nchi.
Jumatano ya tarehe 15 Juni, 2016, Katibu Mkuu wa CUF kupitia
televisheni ya “Voice of America” (VOA), alionekana hadharani akishutumu
Serikali za Tanzania na viongozi wake waliopo na walioondoka madarakani kwa
madai tofauti ya uongo ikiwemo kile alichodai kukosa uwajibikaji na ukiukwaji
wa makusudi wa misingi ya utawala wa sheria.
Kwa maoni ya CCM Zanzibar, jitihada za Maalim Seif hazina lengo
la kutaka kurejewa uchaguzi wa Zanzibar ambao umefanywa kwa mujibu wa sheria za
nchi, bali zinalenga kujitafutia umaarufu alioupoteza kutokana na ubinafsi wake
wa kuwakataza wafuasi wake kushiriki uchaguzi wa marudio, jambo ambalo
limewanyima fursa muhimu kisiasa ya kutoa hoja za kisheria kupitia chombo rasmi
cha kutunga sheria – Baraza la Wawakilishi.
Chama cha Mapinduzi Zanzibar kwa mara nyengine tena kinatoa wito
kwa Serikali zote mbili na vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kuvifumbia macho
vitendo vinavyoendelea kufanywa na kiongozi huyo wa upinzani, kwani athari za
baadae za matukio hayo zinaweza kuwa kubwa kiuchumi, kisiasa, kijamii na bila
ya shaka kwa mustakbali wa maendeleo endelevu ya Zanzibar na
Tanzania kwa jumla.
Aidha, vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kutoa taarifa
kwa umma kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya watu wanaopatikana na
hatia kuhusiana na matukio hayo, vyenginevyo waliowengi wataamini kwamba hakuna
kinachofanyika licha ya hujuma na matukio mengi yanayoendelea kufanywa na hivyo
kuamini kwamba wapo baadhi ya raia ambao wao wapo juu ya sheria.
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinajivunia hali ya amani na
utulivu ambayo imetawala nchini tokea kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,
2015, hadi kumalizika kwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ambao
ulikamilisha ushindi wa CCM kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Tunapongeza uteuzi wa viongozi waliounda Serikali pamoja na
juhudi za Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi kero mbali mbali zinazowakabili
wananchi kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015 – 2020. Kadhalika tunapongeza
hoja mbali mbali zinazotolewa na wajumbe wa CCM kwenye kikao kinachoendelea cha
Bajeti cha Baraza la Wawakilishi.
CCM inawaomba wananchi kutobabaishwa na kauli za uchochezi na
uasi zinazotolewa na Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kuna kila dalili
zinazoonesha kuwa yeye na Chama chake wameshapoteza mwelekeo wa kisiasa na
badala yake wanatafuta mwelekeo mwengine ambao kamwe haukubaliki nchini
Tanzania ambako hakuna historia ya vita wala matukio ya uasi.
Chama Cha Mapinduzi kinawasisitiza wananchi kwamba hakuna
uchaguzi mwengine utakaofanyika kabla ya mwaka 2020 na hakuna Serikali nyengine
itakayekwa madarakani kwa kile kinachodaiwa kumaliza mgogoro wa kisiasa
Zanzibar.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
Sgd.
.....................................
(Waride B. Jabu)
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM
Alkhamis Juni 16, 2016
0 comments:
Post a Comment