WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma amesema Rais
wa Zanzibar ameunda timu ya viongozi na wafanyabiashara wanane kwa ajili
ya kulipatia ufumbuzi tatizo la madawati katika shule za Unguja na
Pemba.
Pembe aliitaja kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Waziri wa Katiba,
Sheria na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, huku wajumbe wengine ni
Waziri wa Fedha na Mipango Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Afya Mahmoud
Thabit Kombo na waziri huyo wa Elimu.
Kamati hiyo inajumuisha Wawakilishi ambao ni wafanyabiashara akiwemo
Mohamed Raza Daramsi, Naila Jidawi na Mohamed Hafidh ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Katika kamati hiyo wamo wafanyabiashara maarufu akiwemo Said Salim
Bahressa pamoja na Seif Nassor Dol ambao kwa pamoja watakuwa na kazi ya
kushajihisha jamii ya makundi mbalimbali kwa ajili ya kupatikana kwa
madawati yatakayotumika katika shule za Zanzibar.
“Hiyo ndiyo kamati iliyoundwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein ambayo imepewa majukumu ya kuhamasisha jamii katika suala zima la
upatikanaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari,” alisema
Pembe.
Alisema serikali imechukua juhudi mbalimbali ikiwemo kuundwa kwa kodi
ya bandari ambayo malengo yake ni kusaidia kupatikana kwa fedha za
madawati. Mikakati inayochukuliwa sasa ni pamoja na wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wote kuchangia Mfuko wa Madawati Sh milioni tatu katika
kipindi cha miezi mitatu.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati Zanzibar, Haroun Ali
Suleiman alisema jumla ya madawati 47,000 yanahitajika kwa shule za
Unguja na Pemba kukabiliana na tatizo hilo. Alisema tatizo la madawati
limesababisha wanafunzi wa shule za Unguja na Pemba kukaa sakafuni.
“Tunahitaji jumla ya madawati 47,000 kwa ajili ya kukabiliana na
tatizo la upungufu wa madawati katika shule zetu Unguja na Pemba ambalo
limewafanya wanafuzi wengi kukaa chini ya sakafu,” alisema. Mapema Raza
ametangaza kuchangia jumla ya madawati 200 kwa niaba ya familia yake
katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo na kuona shule zinakuwa na
madawati ya kutosha
Chanzo Gazei la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment