Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimepiga marufuku ujenzi holela na kazi
mbali mbali za kudumu zinazofanyika katika shamba la Chama hicho bila ya
kujali taratibu za kisheria lililopo Kirombero katika Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kimesema
kuna baadhi ya watu wamevamia shamba hilo na kufanya shughuli za ujenzi
wa nyumba pamoja na kupanda miti ya kudumu ikiwemo minazi na miembe, na
miti mingine ya kudumu bila ya ridhaa halali ya chama hicho.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ndg.
Vuai Ali Vuai wakati akikagua eneo na mipaka ya Shamba hilo huko
Kilombero alisema CCM haitowavumilia baadhi ya watu waliofanya uvamizi
wa kujimilikisha eneo halali la chama hicho bila ya kufuata taratibu za
kisheria.
Alisema
Shamba hilo ni urithi wa Chama cha Afro- Shiraz party (ASP), ambalo
lilinunuliwa na ASP mwaka 1959 kabla ya mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964 kwa ajili ya kuwapati waafrika wazalendo maeneo ya kulima na kuishi baada ya kubaguliwa na kufukuzwa katika mashamba ya watu wengine kwa itikadi za kisiasa.
Vuai
amefafanua kwamba hakuna kiongozi yeyote ndani ya CCM mwenye mamlala ya
kugawa mali yoyote ya chama bali chombo chenye mamlaka hayo ni Baraza
la Wadhamini la CCM ndio linaloweza kutoa ridhaa baada ya kukaa na
kujadiliana na kutoa maamuzi na siyo vinginevyo.
Ameeleza
kwamba chama hicho kitaendelea kuruhusu shughuli za kijamii zifanyike
katika eneo hilo zikiwemo ujenzi wa nyumba za ibada, skuli na visima vya
maji kwa makubaliano na utaratibu maalum unaofaa kisheria lakini siyo
kwa shughuli binafsi.
“ Watu siku hizi wamebadilika na matapeli ni wengi tunaweza kufanya wema wa kuwaruhusu wajenge wachache baadae na
wao wakawakaribisha wengine ama kuuza maeneo hayo jambo linaloweza
kuanzisha migogoro ya ardhi hali ambayo CCM haipo tayari kuona
kinatokea.
Lakini
pia natoa wito kwa watu wote walioanza kujenga na waliokwisha maliza
ujenzi lakini hawajahamia katika nyumba zao na wanaopanda miti ya kudumu
wote wasitishe zoezi hilo mpaka watakapopewa utaratibu mwingine.”,
alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa kama kuna mpango wa kubadili matumizi
ya eneo hilo lazima chama kikae na kujadili kwa kina kisha kitatoa
maamuzi hapo baadae.
Alitoa
onyo kwa baadhi ya watu wanaofanya vitendo vya kitapeli kwa kutumia
hati bandia kwa nia ya kujimilikisha mali za CCM na jumuiya zake kinyume
na sheria na kuwataka kuacha kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai, na
pia kwa Mwana CCM ni kosa kubwa la Kimaadili.
Aidha aliwataka viongozi na watendaji mbali mbali wa Chama hicho nchini, kuanza
utamaduni wa kutembelea na kukagua mali zote zilizokodishwa ama
kumilikishwa na taasisi ama watu ili kubaini vitendo vya udanganyifu na
kuweka mali hizo katika hali ya usalama.
Alisema
kwa busara na hekima za CCM itaweza kuruhusu shughuli ndogo ndogo
ziendelee kufanyika katika eneo hilo zikiwemo kilimo cha mpunga, mboga
mboga na mazao mengine ya muda mfupi, na kuagia viongozi wa ngazi ya
mkoa Kaskazini kwa kushirikiana na viongozi wa chama na serikali katika
shehia ya kilombero kuratibu vizuri shughuli zote zinazofanyika katika
eneo hilo.
Aliwasihi watu
waliopewa dhamana za kulinda mali za chama kuwa makini na kuepuka
kujiingiza katika vitendo vya kitapeli vinavyoweza kuhujumu mali za CCM
na umma kwa ujumla.
Kwa upande wao viongozi wa CCM katika Shehia
hiyo walisema shughuli anazotambua kufanyika katika eneo hilo ni zile
za kijamii zikiwemo skuli na misima vya maji safi pamoja na baadhi ya
watu wachache waliopewa kuishi katika eneo hilo kwa muda na siyo ujenzi
wa nyumba za kudumu.
Viongozi hao walimuahidi Naibu
wa Katibu Mkuu huyo kutekeleza maagizo yote aliyopewa ili kuepusha
migogoro ya ardhi inayoweza kutokea katika eneo hilo kwani CCM ni chama
cha amani kisichotaka wananchi waishi katika matatizo.
0 comments:
Post a Comment