Home » » DKT.SHEIN AWATAWAKA WANACCM KUMUUNGA MKONO.

DKT.SHEIN AWATAWAKA WANACCM KUMUUNGA MKONO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Is-haka Omar, Zanzibar.

MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt.Ali Mohamed Shein amewasihi wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono katika kipindi cha utawala wake wa miaka mitano ili aendelee kusimamia fursa na maslahi ya nchi kwa vitendo.

Alisema maendeleo ya nchi yaliyopatikana kwa miaka mitano iliyopita yametokana na juhudi za wananchi na viongozi mbali mbali wa Chama na serikali walioungana kwa pamoja kufikia mafanikio hayo.

Akizungumza Dkt.Shein na mamia ya viongozi wa CCM wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti na Makatibu wa Matawi na Maskani za Wilaya ya Kaskazini “A” katika mwendelezo wa ziara zake nchini, iliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dkt.Shein alisema suala la kuijenga zanzibar kimaendeleo  ili iendane na hadhi za mataifa mengine hasa nchi za visiwa zilizokuwa kiuchumi na kuimarika  kimaendeleo halina mbadala na linatakiwa kutekelezwa na serikali kwa ushirikiano wa wananchi wote bila kujali tofauti za kidini, kisiasa na kikabila.

 “Nimekula kiapo cha kuwatumikia wananchi wote kwa uadilifu nami naendelea kufanya hivyo, na hakuna mtu wa kunizuia kwani hii ni nchi yetu sote wala si ya mtu wala kikundi fulani na wanaotoa ridhaa ya kuongoza nchi ni nyinyi mlionichagua ili niwaongoze.

Pia naendelea kukuombeni wananchi msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kuivuruga amani ya nchi yetu kwani bado tuna safari ndefu ya kujenga na kuimarisha uchumi wa taifa letu”., alisema Dkt.Shein na kueleza kwamba yeye baada ya kuchaguliwa na wananchi kupitia mchakato halali wa kidemokrasia anakuwa Rais wa wote na sio wa chama kilichomuweka madarakani pekee hivyo kuna haja ya kila mtu kuheshimu sheria na katiba ya nchi.

Dkt.Shein alisisitiza umuhimu wa wananchi kuisoma Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa lengo la kujua haki na miongozo mbali mbali ya kisheria ili kuepuka kufanya makosa ya jinai na madai yanayoweza kuingiza nchi katika machafuko yasiyokuwa ya lazima.

Alisema serikali haitolinda Katiba ya Zanzibar na sheria zake kwa kutumia utawala kibabe na uonevu bali itatenda haki na usawa ili kila mtu atakayevunja miongozo hiyo ahukumiwe kwa mujibu wa kosa alilotenda.

Alifafanua kwamba wafuasi wa CCM toka enzi za ASP na TANU kabla ya kuungana kuwa CCM, hawakuwahi na hawatofanya vitendo vya uhalifu dhidi ya watu wengine kama wanavyofanya wapinzani wa Zanzibar.

Dkt.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar  alisema CCM na serikali hawachukii wala hawana vita na wapinzani kwani nao wanastahiki haki na fursa za nchi kama walivyo watu wengine lakini wasitumie nafasi hizo kuvuruga amani ya nchi.

Alieleza kwamba hatotumia silaha za kivita zikiwemo mizinga na bunduki kuzuia uhalifu unaofanywa na watu wasioitakia mema nchi bali watapambana na vyombo vya dola.

Alikitaja chanzo cha vurugu hizo kuwa zinasimamiwa na Kiongozi Mkuu wa CUF ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Maalim Seif  Sharif Hamad kwa kusaka nafasi ya Urais kwa kutumia njia zisizokuwa halali kwani nafasi hiyo   haipatikani kwa vitisho vurugu na migogoro bali inapatikana kwa kuchaguliwa na wananchi kwa njia ya Kidemokrasia.

“Namshangaa Maalim Seif Sharif Hamad yeye ndiye aliyekataa kurudi katika uchaguzi wa Marudio baada ya ule wa mwanzo kufutwa kwa kasoro zilizojitokeza, laiti angekuwa mshindani angerudi na tukashinda yeye amesusa mimi nimerudi na kushinda badala yake ameanza nongwa na mizengwe ya ya kuhatarisha amani ya nchi”., alieleza Dkt. Shein.

Aidha aliwataka viongozi hao kuwa Mabalozi wazuri wa kuwatuliza na kuwanasaha wanachama wa chama hicho ndani ya Wilaya hiyo wasilipe Visasi wala kujibu mashambulizi ya wapinzani badala yake wafuate taratibu za kisheria kutatua migogoro inayowakabili.

Alisema CCM itaendelea kuenzi kwa vitendo urithi wa Waasisi wa Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964, kwa kuhakikisha kila mwananchi anaendelea kuishi kwa amani na utulivu huku kipato chake kikiongezeka kulingana na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Katika juhudi za kuimarisha Chama hicho Dkt.Shein alitoa Wito kwa makatibu wa Matawi ya CCM kujenga tabia ya kuyafungua kwa wakati na kufanya kazi za chama kwa mujibu wa miongozo na kanuni za Katiba ya Chama hicho ili kujiandaa vyema na uchaguzi mkuu ujao.

Dkt.Shein aliwashukru na kuwapongeza mabalozi hao kwa kwa muamini na kumchagua kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu na hatimaye kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 91.

Pamoja na hayo Dkt. Shein aliahidi kutafuta ufumbuzi wa kumaliza changamoto ya barabara ndani ya Mkoa huo kutoka maeneo ya Mahonda hadi Kivunge, na kuongeza kuwa tatizo lililokuwepo kwa sasa ni upungufu wa vifaa vya kisasa vya ujenzi wa barabara na vikipatika muda wowote itafanyiwa matengenezo.

Kwa upande wa kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira katika Wilaya hiyo, Dkt.Shein alisema serikali kwa sasa imejipanga kufanya mageuzi makubwa ya sekta ya kilimo kwa kuhakikisha vijana wanatumia fursa hiyo kwa kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija ili wapate kujiajiri wenyewe.

Alisema kwamba kiuhalisia ajira zinazotolewa na serikali ni chache na hazikidhi mahitaji ya vijana wote wanaomaliza elimu ya juu na walioishia elimu za msingi na sekondari, hivyo kwa sasa serikali inaendelea kujenga vyuo vya amali na ufundi kwa lengo la kuwapatia vijana ambao hawakupata ajira serikali ujuzi na maarifa ya kujiajiri wenyewe.

Aidha alifafanua kuwa licha ya ajira kuwa kidogo serikalini atahakikisha ajira zinazotolewa zinapatikana kwa misingi ya uwazi na usawa na kuwafikia walengwa ili kupunguza malalamiko ya kuwepo na upendeleo wakati wa kutoa ajira hizo.

Akisoma risala ya Mabalozi hao, Yussuf Shaaban Said alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa na wananchi kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio.

Alisema Mabalozi wa Wilaya hiyo, wataendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kulinda amani na utulivu wa nchi. 

Shaaban alisema kasi ya utendaji wa Dkt.Shein mara baada ya kuingia madarakani sambamba na kuteua Baraza la Mawaziri na viongozi wengine wachapa kazi inaongeza imani na uaminifu kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Mapema Katibu wa Wilaya ya Kaskazini “A” Kichama, Ame Omar Mkadam alisema hali ya kisiasa ndani ya wilaya hiyo inaendelea vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto za wapinzani kupinga na kukosoa kila jambo jema linalofanywa na CCM pamoja na serikali.

Alisema wataendelea kuhamasisha wananchi wa Wilaya hiyo hasa wapinzani kujiunga na chama hicho kwani kimekuwa kimbilio la watu wote huku kikipinga kwa vitendo viashiria vya ubaguzi na uvunjifu wa haki za binadamu.

Kwa upande wa Mabalozi hao, waliiomba serikali kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya Barabara ndani ya Mkoa huo kuanzia maeneo ya Mahonda hadi kivunje ili itengenezwe kwani inategemewa na wananchi wengi.

Pamoja na hayo wameahidi kuendelea kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuuujao wa mwaka 2020.

Pamoja na hayo wameiomba serikali kuendelea kudhibiti vitendo vya ubaguzi na uhalidfu vinavyofanywa na wapinzani toka kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Marudi Zanzibar uliofanyika Machi 20 mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa