Home » » DKT.SHEIN AAPA KULINDA AMANI NA UTULIVU WA Z'BAR.

DKT.SHEIN AAPA KULINDA AMANI NA UTULIVU WA Z'BAR.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

        MAKAMO Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt.Ali Mohamed Shein amesema ataendelea kusimamia vyema amani na utulivu kwa lengo la kuwavutia wawekezaji na mataifa ya kigeni kuwekeza nchini  ili watoe fursa za ajira kwa wananchi.

Dkt.Shein amesema mafanikio hayo yatafikiwa endapo kila mwananchi ataweka mbele uzalendo wa nchi kwa kufanya kazi kwa bidii huku wakilinda amani iliyopo isipotee.

Kauli hiyo Dkt.Shein ameito wakati akizungumza na mamia ya viongozi wa CCM wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti na Makatibu wa Matawi, Maskani, Vijana na Wazee wa chama hicho katika mwendelezo wa ziara zake nchini Wilaya ya Kati kichama Unguja.

Dkt.Shein alisema katika harakati za kuimarisha Uchumi na Maendeleo ya nchi ni lazima kuwepo na amani na utulivu wa kudumu kwani mataifa mbali mbali hayawezi kuwekeza fursa za kiuchumi katika nchi yenye migogoro na vurugu za mara kwa mara.

Alisema malengo ya CCM na serikali kwa ujumla ni kuhakikisha Zanzibar inaimarika kiuchumi sambamba na kuweka ulinzi wa kudumu wa kulinda heshima na hadhi ya nchi inayojaribiwa inayoharibiwa  kwa makusudi na baadhi ya watu wasiohitakia mema Zanzibar.

“Naendelea kusisitiza kwamba serikali haitowavumilia watu wanaokesha wakibuni mikakati na mipango ya kuharibu amani na utulivu wetu, kwani hicho ndiyo chombo cha kutusafirisha na kutufikisha salama katika kilele cha mafanikio kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Wanaccm na wananchi kwa ujumla nakuombeni muendelee kuiamini serikali, kwani italinda kwa gharama yeyote uhuru, usawa, amani na utulivu wenu kwa misingi ya kisheria ”, alisema na kuongeza kuwa maendeleo ya Zanzibar yapo mikononi mwa wananchi wenyewe.

Aidha Dkt. Shein alifafanua kwamba Uchaguzi Mkuu umekwisha wananchi wanatakiwa kuwa wamoja katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo ya nchi.

Alisisitiza umuhimu wa  wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao kufungua ukurasa mpya kwa kujitathimini ni kwa namna gani ataweza kuinusuru nchi yao katika migogoro ya kisiasa.

Aliwataka viongozi wa chama hicho, kujenga utamaduni wa kusoma Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,Katiba ya CCM, miongozo na kanuzi za chama kwa lengo la kuwaelimisha wanachama wengine ili wasipotoshwe na propaganda zinazojengwa na wapinzani.

Akizungumzia changamoto ya ajira nchini alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kupunguza tatizo hilo ikiwemo kufungua milango ya wawekezaji na kushirikisha sekta binafsi.

Alisema kwa sasa serikali ina mpango wa kuanzisha kampuni kubwa ya uvuvi wa Bahari kuu kwa kutumia vifaa vya kisasa pamoja na kuanzisha viwanda vya samaki ili vijana na wananchi kwa ujumla wapate ajira za kudumu.

Alifafanua kwamba mradi huo wa uvuvi utatekelezwa kwa kushirikiana na nchi ya Sir Lanka ambapo kwa awamu ya mwanzo ya majaribio itafanywa katika Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja kwa wavuvi wa maeneo ya Chwaka na Uroa.

Alifafanua zaidi kwa upande wa sekta ya viwanda kwa samaki nchini alisema wakati umefika wa Zanzibar kuja moja ya nchi yenye viwanda hivyo kwani ina rasilimali Bahari yenye samaki wa kutosha na hivi juzi serikali imefanya mazungumzo na wawekezaji kutoka China na wameahidi kuunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande wa sekta ya Afya alisema katika juhudi za kupunguza changamoto za kiafya katika Mkoa kusini serikali ina mpango wa kujenga Hospitali kubwa na ya kisasa kwenye  eneo la Binguni Mkoani humo.

Aliwataka wafusi wa chama hicho kuongeza ari, kasi na juhudi katika kufanya kazi za chama kwani miaka iliyopita baadhi ya wanachama na mabalozi wamekuwa wakijisahau na kupelekea shughuli za chama wakati wa Kampeni za Uchaguzi unakuwa mgumu.

“ Kuna baadhi ya viongozi mnakimbia ofisi za matawi na hamfungui badala yake mnaweka kufuli, na wengine hata wanachama wenu hamuwajui hivyo wenyeviti na makatibu kuanzia sasa fanyeni vikao vyenu kikanuni ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wanachama wetu”., aliagiza Makamo Mwenyekiti huo.

Akimkaribisha Makamo Mwenyekiti huyo, Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema ziara hiyo ni moja ya ahadi zilizotolewa na Dkt.Shein wakati wa kampeni kuwa endapo atashinda katika Uchaguzi mkuu atakutana na viongozi kwa nia ya kuwashukru na kubadilishana mawazo kwa kazi nzuri walioifanya wakati wa uchaguzi.

Vuai alieleza kuridhishwa kwake na hali ya kisiasa iliyopo katika Wilaya ya Kati na kueleza kuwa maeneo hayo yamekuwa ngome na kitovu cha CCM kisiasa.

Akitoa salamu za Mabalozi hao, Imani Suleiman Mgambe walimpongeza Dkt.Shein kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010/2015 na wana matumaini makubwa ya kuongeza kasi hiyo katika utekelezaji wa ilani mpya ya mwaka 2015/2020.

Alisema Wilaya hiyo imepata mafanikio makubwa katika sekta mbali mbali za afya, elimu, umeme na miundombinu ya Barabara kutokana na juhudi na usimamizi na utendaji mzuri wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kwamba Mabalozi na viongozi wa Wilaya hiyo wameahidi kulinda na kukitumikia CCM  ili kiendelee kuwa na nguvu madhubuti na kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo kichama, Hassan Vuai alisema wafuasi wa chama hicho wanaunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar Dkt.Shein kwa kusimamia amani na utulivu wa nchi.

Vuai alisema Wilaya hiyo inalaani vikali hujuma na mateso wanayofanyiwa wafuasi wa chama hicho kisiwani Pemba na kuiomba serikali kuwachukulia hatua watu wote wanaohusika na uhalifu huo.

Mapema Katibu wa Mkoa Kusini Kichama, Sauda Ramadhan Mpambalioto kwa niaba ya mkoa huo amewatunuku tuzo za ushindi na utendaji bora ndani ya CCM viongozi wakuu wa chama ambao ni Mwenyekiti wa CCM Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.

Wengine ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Jonh Pombe Magufuli, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mh.Samia Hassan Suluhu, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mh.Abdulrahman Kinana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mh.Vuai Ali Vuai.

Sauda  alisema viongozi hao wamekuwa mfano wa kuingwa ndani na nje ya chama kwa uadilifu,hekima na busara zao  kiutendaji hasa kusimamia maendeleo ya nchi mijini na vijiji bila ya ubaguzi kwa kipindi kifupi toka waingie madarakani.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa