RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna nchi au jumuiya
za kimataifa zitakazomwondoa madarakani yeye kwa sababu amechaguliwa
kihalali na wananchi kwa kura nyingi kwa mujibu wa Katiba.
Dk Shein alisema hayo wakati akizungumza na wanachama na wafuasi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika matawi ya Wesha Tibirinzi, Pembeni
Shengejuu na Maziwa Ng’ombe, Micheweni katika ziara ya kuwafariji
kutokana na matukio ya hujuma zilizofanywa na wapinzani huko Pemba.
Aliwataka wafuasi wa CCM na wanachama wake waliopo Pemba,
wasibabaishwe na kauli zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa
wanaopita na kudai kwamba uchaguzi mwingine unakuja.
“Mimi ndiye Rais halali wa Zanzibar nimechaguliwa katika uchaguzi
ulioitishwa na Tume ya Uchaguzi... wananchi msisikilize uvumi na kauli
za wapinzani zenye lengo la kuwababaisha na kuwayumbisha katika shughuli
zenu za maendeleo,” alieleza Dk Shein.
Dk Shein alisema amesikitishwa na kauli za uchochezi zinazotolewa na
viongozi wa vyama vya siasa zenye malengo ya kuishajihisha jamii
kutengana na kugombana na kususiana hata katika shughuli za jamii
ikiwemo misiba.
Alisema kiongozi anayefanya vitendo vyenye lengo la kuwagawa wananchi
kwa malengo ya kisiasa kwamba huyo ameishiwa na hana nafasi katika
jamii. “Huyo kiongozi anayewashawishi wananchi kususia shughuli za jamii
na maendeleo basi huyo ameishiwa kisiasa na hana nafasi katika jamii ya
wananchi na ninyi mpuuzeni.
Alikuwa na nafasi ya kushiriki katika uchaguzi lakini alisusa,”
alieleza. Alisema viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wameishiwa hoja
kwa sasa na hawana la kufanya baada ya kugomea kushiriki katika uchaguzi
halali wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambao umetoa nafasi
kwa CCM kushinda katika uchaguzi wa kishindo.
Mapema Dk Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM aliwataka
wanachama wa chama hicho kutembea kifua mbele na kuachana na unyonge kwa
sababu chama chao ndiyo kilichoshika dola na kuunda serikali.
Akizungumzia yanayotokea Pemba, Dk Shein alisema, “Nimesikitishwa na
taarifa za matukio mbalimbali yanayofanyika huku Pemba ikiwemo watu
kususiwa maiti, kushushwa katika gari za abiria baada ya kuwa na itikadi
tofauti......haya matukio hayakubaliki na yanakwenda kinyume cha
maamrisho ya dini zote.”
Aliwataka viongozi waliopewa majukumu kwa mujibu wa Katiba kufanya
kazi zao na kupambana na vitendo vya ubaguzi ikiwemo vya kuonewa
kiholela wananchi.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment