NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali
Vuai amewapongeza wanachama wa chama hicho Pemba kwa kuonesha uvumilivu
wa hali ya juu tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 na
kuendelea kukiamini chama hicho.
Vuai alisema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM Wesha,
Tibirinzi Pemba na kusema uvumilivu wa wana CCM Pemba, unastahiki
pongezi za hali ya juu. Alisema matukio yanayofanyika sasa, ikiwemo wana
CCM kususiwa na kushushwa katika gari za abiria na wengine kususiwa
maiti, ni sehemu ya vitimbwi vinavyofanywa na wapinzani wakiwa na lengo
la kuona nchi haitawaliki.
“Tunawapongeza kwa dhati kabisa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi pamoja
na wanachama wake kwa kuonesha uvumilivu wa hali ya juu katika
kupambana na matukio ya vitendo vya udhalilishaji yanayokwenda kinyume
cha maadili ya utu na ubinadamu,” alisema Vuai.
Aliwataka kuwa wastahimilivu na kufanya kazi kwa mshikamano mkubwa
kwa sababu juhudi zao zimeonekana, ambazo zimekifanya chama hicho kuwepo
madarakani. Baadhi ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi, wameitaka
serikali iliyopo madarakani ya CCM kupambana na vitendo vya hujuma,
vinavyofanywa na wapinzani wanaodai kwamba ‘wanaisubiri serikali yao
kuingia madarakani’.
Risala iliyosomwa na Katibu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Mafunda
Khamis, ilisema vitimbi vinavyofanywa na wapinzani lengo lake kubwa
kuona Pemba ‘haitawaliki’. “Hawa wapinzani lengo lao kubwa kuona nchi
haitawaliki kama anavyodai kiongozi wao wa upinzani,” alisema Khamis.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment