Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akimkabidhi vifaa mkulima Trekta ndogo ya mkono (Power tillers) aliyevaa fulana ya rangi ya njano na kofia na wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Zanzibar Nadir Abdul-Latif Yussuf aliyetoa vifaa hivyo kwa wananchi hao.
baadhi ya wananchi na viongozi waliofika katika hafla fupi ya makabidhiano ya matrekta (Power tillers) mbili na mashine moja ya umeme wa jua(solar).
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka wabunge, wawakilishi na madiwani kuhakikisha miradi wanayopeleka majimboni inawanufaisha wananchi wote. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Mabodi wakati akikabidhi matrekta madogo ya mkono (Power tillers) mbili na mashine ya umeme wa solar moja kwa wakulima wa jimbo la Chaani zilizotolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Nadir Abdul-Latif Yussuf.
Dkt. Mabodi alisema ahadi zinazotekelezwa na viongozi mbali mbali wa majimbo nchini ni lazima ziwanufaishe wananchi wote ili kufikia malengo ya mapinduzi kwa vitendo. Alieleza kuwa vifaa hivyo vya kilimo vilivyotolewa na mwakilishi huyo vinatakiwa kutumiwa vizuri na wakulima ili visaidie shughuli za kilimo katika jimbo hilo.
Aidha Dkt. Mabodi aliwasisitiza viongozi na watendaji wapya waliochaguliwa katika uchaguzi unaoendelea hivi sasa ndani ya chama na jumuiya zake kufanya kazi za taasisi hiyo kwa bidii ili chama hicho kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
“ Nawapongeza viongozi wanaotekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kasi ili wananchi waweze kunufaika na fursa mbali mbali za maendeleo zinazofanywa na viongozi wao.”, alisema Mabodi.
Naye Mwakilishi wa Jimbo hilo , Nadir Abdul-Latif Yussuf alisema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa vyenye thamani ya shilingi milioni 21 ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi wa jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita. Nadir aliwapongeza wananchi wa jimbo hilo kwa kumuunga mkono katika masuala mbali mbali ya kijamii hali inayompa nguvu za kuendelea kutatua kero zinazowakabili katika nyanja za kijamii na kiuchumi.
Alisema lengo la kutoa vifaa hivyo kwa wananchi wa jimbo hilo ni kupunguza changamoto za upungufu wa pembe jeo za kilimo zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa jimbo hilo kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment