Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 09.08.2017
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja kwa Shirika la Utangazaji
Zanzibar (ZBC) kujiendesha kibiashara ili lizidi kuimarika sambamba na kutekeleza
azma ya kutoa elimu kwa umma.
Dk. Shein alieleza hayo
leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo pamoja
na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Uongozi wa Shirika
hilo katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alisema kuwa lazima Shirika liendeshwe kibiashara kwa lengo la kuweza
kupata faida ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zinazopaswa kutolewa malipo
zisitolewe bure ili Shirika hilo liweze kujiimarisha vyema.
Dk. Shein, aliongeza kuwa lengo
na madhumuni ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kulibadilisha Shirika hilo
na ndio maana juhudi kubwa zimechukuliwa katika kufikia lengo lililokusudiwa na
hivi sasa limeanza kupata mafanikio na hasa pale baada ya kufanya ziara zake
katika kituo cha Redio na Televisheni na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kuona
mafanikio yaliopatikana.
Aidha, Dk. Shein alisema
kuwa Zanzibar ina historia kubwa kwenye vyombo vya habari vya redio na
televisheni katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ambapo iliweza
kujijengea sifa kubwa na kupelekea wahusika wa kada hiyo kutoka nje na ndani ya
nchi waje kujifunza hapa Zanzibar.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kusisitiza umuhimu wa mabadiliko katika Shirika hilo na kueleza kuwa
Shirika haliwezi kufanya vizuri iwapo hakutakuwa na mabadiliko. Hivyo, aliungana
na viongozi wengine katika kikao hicho kwa kulipongeza Shirika la ZBC pamoja na
uongozi wake ukiwemo uongozi wa Wizara kwa kuonesha mabadiliko ya kweli huku
akisisitiza suala zima la uzalendo,mashirikiano na mapenzi miongoni mwao.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa miongoni mwa vitegemezi vya uchumi wa Zanzibar ni karafuu na
ndio maana Serikali anayoiongoza baada tu ya kuingia madarakani ikalipa
kipaumbele zao la karafuu kwa kupandisha bei ya zao hilo, hivyo alilitaka
Shirika la ZBC kuwa mstari wa mbele kulitangaza zao la karafuu.
Aliongeza kuwa lengo kubwa
la Shirika hilo ni kutoa elimu kwa umaa kupitia televisheni na redio, hivyo ni
vyema likawaelimisha wananchi juu ya zao la karafuu na kusisitiza haja ya
mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji wa Shirika hilo.
Alieleza kuvutiwa kwake na
jitihada za ZBC katika kuandaa vipindi vipya vya redio na televisheni sambamba
na ubunifu ulioanzishwa na Shirika hilo katika kubuni vipindi mbali mbali vya
kuelimisha, kufunza na kuburudisha.
Mapema Makamo wa Pili wa
Rais Balozi Seif Ali Idd alitoa pongezi kwa kazi nzuri inazozifanya Shirika
hilo sambamba na juhudi inazozichukua kutoka katika mfumo wa analogi kwenda
digitali.
Nae Waziri wa Habari,
Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alieleza aliahidi kuwa ZBC
itaendelea kusimamia juhudi za Dk. Shein ya kuhakikisha Shirika hilo
linaimarika huku akieleza kuwa ZBC ina dhima ya kuonesha na kutangaza vipindi
vya maendeleo mbali mbali likiwemo zao la karafuu.
Naibu Waziri wa Wizara
hiyo, Chumu Kombo Khamis alieleza haja kwa Wawakilishi kisiwani Pemba kulitumia
vyema Shirika la ZBC kwa kueleza mambo wanayoyafanya.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi
na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisisitiza haja ya
kuandaliwa mapema mpango wa kuwapata wataalamu katika Shirika hilo hasa
ikizingauiwa kuwa baadhi ya wataalamu wamekuwa wakistaafu.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya ZBC, Bi Nasra Mohammed alieleza mafanikio na changamoto za ZBC
huku akieleza juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Bodi yake ya kufanya ziara
katika vituo mbali mbali vya televisheni pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa
Shirika hilo wanaofanya kazi zao mjini
Dar-es-Salaam.
Nao uongozi wa ZBC ulitoa
pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia mitambo ya kisasa,
kubadilisha haiba ya studio za ZBC Radio, mafanikio ambayo yameoneshwa na Dk.
Shein katika umahiri wake wa kutimiza lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya
mwaka 2015-2020.
Aliongeza kuwa ZBC imeweza
kununua (sever) ili kuhifadhi hotuba za viongozi wa kitaifa, nyimbo za zamani
katika mfumo wa kisasa na uhifadhi uliobora zaidi huku akieleza kuwa ZBC Radio
kwa sasa imeweka website (www.zbc.co.tz) kwa
majaribio na hadi sasa jumla ya wasikilizaji 8000 wanasikiliza ZBC Redio
kupitia njia hiyo.
Wakati
huo huo,
Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Bodi
ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) na uongozi wake na
kupongeza mafanikio yaliofikiwa katika kipindi kifupi tokea kuundwa kwa cha
Taasisi hiyo.
Nae Kaimu Waziri wa Wizara
hiyo, Ali Abeid Karume alieleza umuhimu wa kuundwa kwa taasisi hiyo ambayo
itasaidia katika kusimamia viwango vya bidhaa zinazozalishwa ama kuingia
Zanzibar hatua ambayo itasaidia kuwalinda watumiaji.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi
hiyo Profesa Ali Seif Mshimba alieleza kuwa madhumuni makubwa ya shughuli za
ZBS ni kulinda afya na usalama kwa watumiaji wa bidhaa na huduma, kuhifadhi
mazingira ya nchi na kushajiisha ukuaji uchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa
zenye ubora viwandani na kilimo na biashara ya kimataifa.
Alieleza Dira ya ZBS kuwa
ni kufikia kuwa miongoni mwa Taasisi za Viwango Duniani katika kuweka viwango
na kutoa huduma za udhibiti, ubora na vipimo vinavyokubalika na kuheshimika.
Nao uongozi wa ZBS
ulieleza kuwa jumla ya kampuni 24 zimewasilisha maombi ya kutumia alama ya
ubora ya ZBS ambapo bidhaa 31 zimeombewa matumizi ya alama ya ubora na 10
zimepewa cheti cha matumizi ya alama ya ZBS ambapo kati ya hizo 6 za ndani na 4
za nje ya nchi na bidhaa 21 zinaendelea na hatua za kuthibitishwa ubora.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
0 comments:
Post a Comment