Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Kautahr Ishaka, Maelezo, Pemba
Umaarufu
na umuhimu wa zao la karafuu unazidi kuongezeka Zanzibar, siku hadi
siku, hasa katika awamu hii ya saba, kutokana na jitihada maalum
zinazochukuliwa na Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein,na
viongozi mbali mbali, wakiwemo Mawaziri, Makatibu wakuu, Wakuu wa Mikoa,
Wakuu wa wilaya pamoja na Wafanyakazi wote wa ZSTC wakiongozwa na
Mkurugenzi Mwendeshaji.
Serikali kwa kuhakikisha kuwa lengo hilo la kuwanufaisha wakulima na
Wadau wa zao la karafuu linatekelezwa vyema, ikaamua kuwa miongoni mwa
kazi za Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ziwe ni hizi zifuatazo, ambazo
zitamsaidia mkulima na mdau wa zao la karafuu moja kwa moja.
Kufanya usajili wa Wakulima wanaomiliki na wanaokodi mashamba ya
mikarafuu ili kurahisisha shughuli za utoaji wa huduma, Kusaidia miradi
ya maendeleo ya miundo mbinu katika maeneo yenye mashamba ya mikarafuu,
kutoa mikopo ya fedha taslimu kwa Wakulima na Wanaokodi karafuu kwa
hatua za awali za uchumaji wa karafuu na ununuzi wa majamvi kwa kuanikia
kuwakatia bima wachumaji wa karafuu watakaopata ajali wakati wakichuma
karafuu.
Mkurugenzi Fedha wa ZSTC, Bwana Ismail Omar Bai, akifafanua Msimu wa
mwaka 2016/17 alisema , ulikuwa ni msimu mdogo ukilinganisha na msimu
uliopita (2015/16), manunuzi ya karafuu yalianza mapema katika mwezi wa
Julai na yaliendelea vizuri katika kipindi chote cha manunuzi.
Makisio ya vuno la mwaka mzima ilikuwa ni tani 2,810 ambapo manunuzi
makubwa yalitarajiwa kupatikana katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi
Novemba 2016.
Alisema Shirika liliendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na Wadau wote
katika harakati za kuendeleza juhudi za Serikali katika kuhakikisha
kwamba Sekta ya karafuu inakuwa endelevu.
Aidha, kutokana na mashirikiano hayo kutoka kwa Wadau mbali mbali
Shirika liliendelea kufanya kazi kwa mafanikio makubwa ambapo Shirika
kwa mwaka huu hadi kufikia tarehe 30/04/2017 limeshanunua karafuu jumla
ya tani 2,266.2 zenye thamani ya Tzs 31.8 bilioni Kutoka kwa Wakulima
Unguja na Pemba (Unguja tani 132.5 kwa thamani ya Tzs1.8 bilioni na
Pemba tani 2,133.7 kwa thamani ya 29.9 bilioni.
Manunuzi hayo ni sawa na asilimia themanini na moja (81%) ya
makadirio yaliyowekwa kwa mwaka 2016/2017, makadirio kwa mwaka ilikuwa
ni kununua tani 2,810 za Karafuu, ambapo Unguja tani 160.0 na Pemba
2,650.0.
Afisa Mdhamini wa ZSTC Pemba, Abdalla Ali Usi alisema Shirika hilo la
biashara limeonekana wazi kuwa limekuwa likifanya kazi zake kwa
mafanikio makubwa hivyo haliko nyuma katika kutoa huduma za kijamii kila
pale inapopata nafasi ikiwa linatoa misaada katika sekta ya Afya,Elimu
na shughuli za kijamii,
ZSTC imefanikiwa kusaidia kutoa msaada wa madawati kwa skuli za Kisiwa
Panza,Uweleni na Mjimbini huku ikitoa gari za kupakilia wagonjwa Mkoa wa
Kusini Pemba pamoja na vituo vyake vyote kutumika katika shughuli kama
maziko,maulidi na harusi vijijini.
Tujitahidi kupanda miche ya mikarafuu kwa wingi na kuihudumia sifa na
ubora unahitaji kuimarishwa kwa kutumika vigezo vyote kuanzia kuchuma,
kuzichambua na kuanika kwa kutumia vifaa vinavyopaswa kutumika kwa kazi
hizo.
Serikali ione ziada ya thamani ya wakulima wetu kwani “WAKULIMA WETU
NDIO HAZINA YETU” bila ya mkulima wa karafuu hakuna mashamba ya
mikarafuu na wala ZSTC hawataweza kununua karafuu hivyo, nguvu za
makusudi za kumkomboa mkulima wa karafuu ziendelee kuwa endelevu ili
kuwaneemesha wakulima wetu, jamii yetu na Taifa kwa ujumla.
Tuendeleze jitihada za Serikali, tuendeleze mshikamano uliopo wa kupiga
vita usafirishaji wa karafuu na miti ya mikarafuu kwa magendo kwani
kufanya hivyo ni kuua uchumi wa Nchi.
Zao hili ni lenye faida kubwa kwetu, tulitunze kwa kuhakikisha uvunaji
hauleti taathira katika miti na kusababisha miti kupunguza uzazi,
tujitahidi katika kuhakikisha uzalishaji unafuata vigezo vyote vya
ubora ili sifa ya karafuu za Zanzibar ibaki ulimwenguni kote.
0 comments:
Post a Comment