MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Wahujumu wa Uchumi
Zanzibar (ZAECA), imesema wizara tisa za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ) pamoja na watendaji wake wamebainika kufanya vitendo vya
ubadhirifu wa fedha za umma.
Ofisa uchunguzi katika taasisi hiyo, Khamis Bakari alisema Sh bilioni
1.6 zimebainika kupotea katika wizara hizo pamoja na taasisi za vikosi
vya ulinzi vya SMZ. Bakari alisema kazi inayofanywa kwa sasa ni
kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha majalada ya kesi kwa Mkurugenzi wa
Mashtaka na Makosa ya Jinai Zanzibar (DPP). “Tumemaliza uchunguzi katika
hatua ya mwisho na sasa tunakusudia kuwasilisha majalada ya kesi katika
Ofisi DPP kwa hatua nyingine zaidi,” alisema.
Alizitaja wizara ambazo watendaji wake katika Idara ya uhasibu
kuhusika na tuhuma hizo ni Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Afya,
Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko pamoja na Wizara ya Habari,
Utangazaji, Utalii na Michezo.
Aidha alisema katika ubadhirifu huo vipo vikosi vya Idara ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ambavyo ni KMKM, JKU pamoja na Chuo cha
Mafunzo Zanzibar. Mwishoni mwa wiki Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Khalid Salum Mohamed akizungumza na wandishi wa habari alikiri kuwepo
kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha huku watendaji 21 wakihusishwa na shutuma
hizo. Alisema madai yote ya ubadhirifu wa mali ya umma kwa watumishi wa
serikali yamepelekwa kwa mamlaka ya rushwa na sasa yapo katika hatua za
mwisho kufikishwa Mahakamani kwa ajili ya kufunguliwa kesi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment