Home » » Dk Shein aahidi kuvutia uwekezaji

Dk Shein aahidi kuvutia uwekezaji


RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema Serikali yake imedhamiria kuitilia mkazo na kuiimarisha sekta ya uwekezaji ambayo matunda yake yatawasaidia wananchi wote wa Zanzibar.
Ameyasema hayo jana alipofanya mahojiano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali mara baada ya kumaliza ziara yake ya kuitembelea miradi ya Kampuni ya Bakhresa ikiwemo ujenzi wa nyumba 600 huko Fumba pamoja na ujenzi wa hoteli ya kisasa huko Mtoni mjini Zanzibar.
Alisema mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za kisasa huko Fumba utasaidia kwa kiasi kikubwa kutokana na Serikali kuweza kupata pato sambamba na wananchi wa Fumba na maeneo jirani kuweza kupata ajira.
“Fumba ilikuwa imefumba, lakini hivi sasa itafumbuka kwani kukamilika kwa mradi huu Fumba itakuwa ni sehemu ya pekee katika kukuza uchumi wetu pamoja na kuwasaidia wananchi wote kutokana na pato litakalopatikana katika maradi huo,” alisema Dk Shein.
Alisema matarajio ya ujenzi huo ambao kwa maelezo ya uongozi wa kampuni hiyo, eneo hilo litakuwa ni Dubai ya Zanzibar linatoa matumaini makubwa katika kuuimarisha uchumi wa Zanzibar, ambapo mradi huo utajulikana kwa jina la ‘Uptown Living’.
Aidha, alisema nchi nyingi duniani zilianza na miradi kama hiyo ambazo zilikuwa ni masikini kuliko Zanzibar, lakini hivi sasa zimepiga hatua kubwa na kuwa nchi tajiri kutokana na kuwepo miradi kama hiyo na kueleza kuwa kinachofanywa na serikali katika suala zima la uwekezaji ni tija kwa wananchi wote.
Kutokana na juhudi hizo, Dk Shein alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuheshimu na kufuata taratibu zote zilizowekwa na Serikali juu ya suala zima la matumizi ya ardhi.
Katika maelezo yake, Dk Shein alisikitishwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuvunja sheria na taratibu zilizowekwa juu ya umiliki wa ardhi huku wakitambua kuwa ardhi ni mali ya serikali hivyo kila mmoja ana jukumu la kuilinda na kuitunza ardhi iliyopo. Kwa upande changamoto ya ajira kwa vijana wa Zanzibar hasa katika sekta ya utalii, alisema jambo muhimu ambalo litawapa vijana wa Zanzibar ajira kwa haraka katika sekta hiyo ni kuwa na elimu ya fani hiyo.
Alisema kuwa suala la elimu ni muhimu sana na kutoa wito kwa vijana wa Zanzibar kujikita zaidi katika kujitafutia elimu na ndio maana Serikali anayoiongoza imeweza kutilia mkazo suala hilo kwa kukiimarisha Chuo chake cha Huduma za Watalii kiliopo Maruhubi kwa kutoa mafunzo ya Cheti, Diploma huku kukiwa na mchakato wa kukiingiza kuwa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Mapema, Dk Shein alitembelea mradi ya nyumba za kisasa akiwa na mwenyeji wake, mfanyabiashara maarufu Said Salim Bakhresa na kupata maelezo juu ya uendelezaji wa mradi huo unaoanza na nyumba 92 za kisasa zinazoendelea kujengwa ambazo zitakuwa kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha juu na kipato cha kati.
Mradi huo ambao mbali ya nyumba utakuwa na eneo maalumu la bustani kwa ajili ya wananchi, bandari ambayo itawasafirisha wakazi wa eneo hilo kutoka eneo hilo hadi Dar es Salaam kwa boti maalumu zitakazokuwepo eneo hilo huku uongozi huo ukieleza hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha suala ziama la ulinzi na usalama linaimarishwa.
Pia, Dk Shein alipata fursa ya kuangalia mtambo wa kisasa wa kupikia lami unaomilikiwa na Kampuni hiyo ya Bakhresa na baadaye kukagua barabara itakayotoka eneo hilo hadi uwanja wa ndege.
Ziara ya Dk Shein ilimalizika huko Mtoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo alijionea ujenzi wa hoteli hiyo itakayokuwa na sifa ya kimazingira ‘Eco Friend’ ambayo inajengwa kwa umiliki wa kampuni hiyo ambayo inatarajiwa itakuwa ni ya pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa ujenzi wa mradi huo Salim Aziz, alisema kuwa hoteli hiyo itajitosheleza kwa huduma za maji na umeme na kupunguza gharama katika matumizi hayo.
Sambamba na hayo, Dk Shein alitembelea eneo la bahari kuona shughuli za ufukiaji bahari lenye ukubwa wa heka 4 ambalo ni eneo la hoteli hiyo linalotarajiwa kuwa na maegesho ya meli ndogo na meli kubwa, huduma za bustani ya maji ambayo inajumuisha michezo ya kila aina itakayochezwa na wananchi pamoja na watalii.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa