VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwamo Wabunge, Wawakilishi
pamoja na Madiwani, wametakiwa kutekeleza Ilani ya CCM ili kuhakikisha
CCM inashinda katika uchaguzi ujao.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya CCM, Idara ya Itikadi
na Uenezi ya CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, wakati akizungumza na
wanachama wa chama hicho huko Bumbwini Misufini, katika mkoa wa
Kaskazini B, Unguja.
Jabu alisema, CCM imechaguliwa na wananchi kushika nafasi ya kuongoza
serikali ambapo hatua hiyo inaonesha wazi kwamba wananchi wameridhika
na kujenga imani dhidi ya chama hicho kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.
Alisema viongozi hawana budi kutekeleza Ilani ya chama ya mwaka
2016-2020, pamoja na ahadi za viongozi hao walizotoa katika majimbo ya
uchaguzi.
“Chama Cha Mapinduzi kimepewa ridhaa ya kuongoza nchi katika uchaguzi
wa mwaka jana, ambapo viongozi wajibu wao mkubwa, ni kutekeleza kwa
vitendo ilani pamoja na ahadi zote walizotoa kwa wananchi na wanachama,”
alisema.
Jabu alisema kwa kiasi kikubwa CCM, imeridhishwa na juhudi
zinazochukuliwa na viongozi wa majimbo ya uchaguzi katika kutekeleza na
kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miradi ya maji safi na
salama na ujenzi wa shule za msingi.
Awali, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Haji Mkema, amewataka
wanachama kuimarisha chama kwa kulipia kadi za uanachama kwa wakati
pamoja na kupeperusha bendera za chama katika matawi ya CCM.
Alisema kulipia kadi kwa wakati ndio uhai wa CCM katika majimbo ya
uchaguzi ambao utasaidia kuongeza ari kwa wananchi wa kawaida kujiunga
na chama hicho.
“Viongozi wa CCM fanyeni kazi ya kuhamasisha wanachama kulipa ada za
uanachama kwa wakati pamoja na kuweka bendera za chama katika matawi au
sehemu za mabalozi,” alisema.
Mkema aliwahakikishia wanachama kwamba uchaguzi umekwisha na
utafanyika mwingine ifikapo 2020 na kazi kubwa iliyopo ni kuimarisha
chama ikiwemo kuingiza wanachama wapya kupitia katika jumuiya za chama.
CHANZO GAZETI LAHABARI LEO
0 comments:
Post a Comment