WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imesema ipo katika mchakato wa
kuajiri jumla ya walimu wapya 70 wa masomo ya sayansi ikiwa ni sehemu ya
mikakati ya kuondosha tatizo la uhaba wa walimu wa kada hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri,
alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu juhudi zinazochukuliwa
katika kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya
sayansi.
Alizitaja juhudi zilizochukuliwa katika hatua ya awali ni pamoja na
wizara kuwasiliana na Kamisheni ya Utumishi Serikalini ambayo imetoa
kibali cha kuajiri walimu wapya wa masomo ya sayansi.
“Tupo katika mchakato wa kuajiri walimu wa masomo ya sayansi ambapo
kwa sasa tumepata kibali kutoka Tume ya Utumishi Serikalini kufanya kazi
hiyo,” alisema.
Alisema katika hatua ya awali wataajiri walimu 900, lakini kwa sasa wamepewa kibali cha kuajiri walimu 70 wa masomo ya sayansi.
Alisema kwa sasa walimu hao wataajiriwa kwa ajili ya masomo ya
sayansi ambapo wapo katika hatua za mwisho za kufanyiwa udahili kwa
ajili ya kazi hiyo.
Mjawiri alisema kuajiriwa kwa walimu hao kwa kiasi kikubwa kutasaidia
kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi
wanaohitajika katika shule mbalimbali za Unguja na Pemba.
Alisema kuajiriwa kwa walimu hao kutakwenda sambamba na mikakati ya
Wizara ya Elimu ya kuimarisha maabara ya masomo ya sayansi zinazojengwa
katika shule za sekondari Unguja na Pemba.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inakabiliwa na uhaba mkubwa wa
walimu wa masomo ya sayansi kiasi cha kulazimika kuomba msaada kupata
walimu kutoka nchini Nigeria.
CHANZO GAZETI LAHABARI LEO
0 comments:
Post a Comment